Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki ya dunia na Serikali kuendelea kuboresha Mahakama nchini

Mahakama Benki.jpeg Jaji Mkuu wa Tanzania akipokea maelezo toka kwa DC wa Nyasa wakati wa ziara hiyo

Tue, 1 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,imesaini makubaliano na Benki ya Dunia kuendelea kuifadhili Mahakama ya Tanzania katika kuboresha miundombinu ya majengo katika awamu ya pili.

Katika makubaliano hayo, Mahakama inatarajia kujenga vituo jumuishi vingine vya Utoaji haki tisa katika mikoa isiyo na majengo ya Mahakama Kuu pamoja na Mahakama za Mwanzo 60 hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, wakati akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Nyasa akiwa katika ziara yake mkoani Ruvuma kuongea na watumishi na kuangalia maboresho ya miundombinu ya Mahakama iliyofanyika katika kipindi cha miaka mitano.

Alisema,hivi sasa ya Serikali na Benki ya Dunia zipo katika awamu ya mwisho ya makubaliano, ambapo maboresho hayo yatasaidia sana kumaliza baadhi changamoto ikiwamo majengo na miundombinu mbalimbali katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Jaji Mkuu,ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha ambazo zimewezesha kufanya maboresho na mabadiliko makubwa ya Mahakama nchini katika muda wa miaka mitano iliyopita.

Amewataka watumishi wa Mahakama wilayani humo,kuendelea kuchapa kazi kuzingatia maadili na weledi mkubwa wakati wa kusikiliza mashauri na kutoa hukumu mbalimbali ili kuepuka malalamiko yasio ya lazima kutoka kwa jamii.

Aidha,ameipongeza Mahakama ya wilaya ya Nyasa kwa kufanikiwa kuondosha(kusikiliza)mashauri kwa asilimia 88 kuanzia Mwezi Januari hadi Disemba 2021 licha ya wilaya hiyo kuwa na Hakimu mmoja,huku Mahakama ya za Mwanzo zikifanikiwa kumaliza mashauri yaliyofikishwa kwa asilimia 97.

Amewapongeza watumishi wa Mahakama katika wilaya ya Nyasa kwa kazi nzuri wanayofanya,lakini amewataka kujiandaa na mabadiliko na matumizi ya Tehama katika utendaji wa kazi za kila siku badala ya utaratibu wa zamani wa kutumia karatasi.

Alisema,kwa sasa Mahakama hapa nchini ina upungufu wa watumishi takribani laki sita,lakini kwa kutumia mfumo waTehama utasaidia kupunguza pengo hilo na kuwataka kujiendeleza kielimu ili kwenda sambamba na mabadiliko makubwa yanayofanywa na Mahakama.

Katika hatua nyingine Jaji Mkuu alisema,kuanzia mwezi Juni mwaka huu Serikali inatarajia kujenga majengo ya Mahakama katika wilaya mbalimbali hapa nchini ikiwamo wilaya Nyasa kwa ajili ya kutoa huduma za Kimahakama kwa watumishi na wananchi.

Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea Geofrey Mashafi alisema,Halmashauri ya wilaya ya Nyasa imeshatoa kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 16,920 tangu mwaka 2017 ambacho kinafaa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya wilaya.

Kwa mujibu wa Mashafi, kwa sasa jengo linalotumika kama Mahakama ya wilaya ya Nyasa ni la kukodi la halipo katika hali nzuri,hivyo amemuomba Jaji Mkuu kutoa kipaumbele suala la ujenzi wa Mahakama katika wilaya hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Nyasa Kanal Raban Thomas alisema,kama Serikali itajenga jengo la kisasa la Mahakama katika wilaya hiyo itasaidia kuwapunguza wananchi usumbufu wa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta haki. Kanali Thomas alisema, kama Serikali wanatakiwa kutenda haki na watahakikisha haki inapatikana kutoka kwenye vyombo na watumishi waliopewa dhamana na wajibu wa kutenda na kutoka haki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live