Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya nyama yapaa Dodoma, uhaba wa ng’ombe watajwa

Nyama Za Ng'ombe Bei ya nyama yapaa Dodoma, uhaba wa ng’ombe watajwa

Thu, 5 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Bei ya nyama ya ng'ombe kwenye baadhi ya mabucha katika jijini la Dodoma imepanda kutoka Sh7,000 hadi Sh10,0000 kwa kilo huku moja sababu ikitajwa kuwa ni uhaba wa ng’ombe minadani mkoani Dodoma.

Wakizungumza na Mwananchi leo Alhamisi ya Januari 5, 2023 jijini hapa, wamiliki wa mabucha wamesema kwa sasa biashara ni mbaya kwani minada ya Kizota na Msalato mkoani Dodoma kuna uhaba wa ng’ombe na hata wakipatikana bei zipo juu.

Shaban Juma, mmiliki wa mabucha ya Shebby, amesema licha ya kuadimika, lakini ng'ombe mwenye kilo 60 anauzwa kwa zaidi ya Sh700,000 hali inayowapa wakati mgumu.

“Tumekubaliana kupandisha bei ili na sisi tupate kitu kidogo, lakini biashara imekuwa mbaya kwetu, wanunuzi wa nyama wamekuwa wachache,” amesema Juma.

Amesema kwa sasa wamekuwa wakilazimika kuwafuata wafugaji vijijini katika maeneo ya Bahi na Chemba ambao pia wanauza kwa gharama kubwa.

Francis John, mmiliki wa mabucha ya Francis amesema sababu ya kuadimika kwa ng'ombe ni kutokana na wafugaji wengi kusafirisha mifugo kwenda Dar es Salaam.

“Bei imepanda pia kutokana na kupanda kwa gharama za usafirishaji kutoka vijijini hadi kwenye minada, zamani ilikuwa ni kuswaga tu mpaka machinjio au minadani.

“Sasa hivi waswagaji wanataka mpaka Sh20,000 kwa ng’ombe mmoja,” amesema John.

Kwa upande wake, muuzaji wa nyama katika eneo la Sabasaba, Ramadhan Elius amesema awali walikuwa wakiuza kwa Sh6,000 mpaka Sh7,000 lakini sasa imepanda hadi Sh9,000.

“Kimsingi tunakoelekea huenda ikapanda zaidi kwani wafanyabiashara wa nyama wanalalamikia ng'ombe kuadimika na hata wakiwapata wanakuwa hawana ubora unaotakiwa,” amesema.

Muuza mishkaki, Said Juma amesema amepandisha bei ya mishkaki kutoka Sh500 hadi Sh1,000 kutokana na ongezeko la bei hizo.

“Wateja wamepungua sana kwa sababu hawakubali kuuziwa kwa Sh1,000, ongezeko hili linatuumiza sisi ambao tunatafuta riziki kupitia nyama,” amesema Juma.

Naye mama lishe, Rehema Mwanyobe amesema kupanda kwa bei kunawapa wakati mgumu wateja wao kwani wamepunguza ukubwa wa kipande cha nyama.

“Hiyo inawafanya wateja waone kama vile tunawapunja, lakini ukweli ndio huo tunakata vipande vidogo vidogo,” amesema mama lishe huyo.

Mariamu Kiswagala ambaye ni mama wa nyumbani amesema kupanda kwa bei kumewafanya waanze kununua nyama nusu kilo badala ya kilo moja.

“Mume wangu alikuwa akiniachia Sh10,000 ninunue kilo moja, viungo na mboga za majani sasa hivi inashindikana,” amesema Mariamu.

Chanzo: Mwananchi