Baraza la Wazee Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro wameeleza kuridhishwa na utendaji wa viongozi wa serikali wilayani humo hasa katika usimamizi wa Miradi ya maendeleo na kuboresha huduma pia kutafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali ikiwemo mapambano dhidi ya biashara haramu ya Dawa za kulevya.
Wakizungumza wakati wa hafla iliyoandaliwa na Baraza hilo maalum kumpongeza mkuu wa Wilaya hiyo ya Same Kasilda Mgeni Wajumbe wa Baraza hilo wamesema kwa muda mfupi tangu kuteuliwa kwake kuwa mkuu wa Wilaya ya Same kiongozi huyo ameonesha Ushupavu,Ujasiri na uhodari kwenye uwajibikaji kwa kuchukua hatua stahiki kwa wakati.
Mwenyekiti wa Baraza hilo la Wazee Timoth Mgonja amesema kilichowasukuka kuandaa hafla ya kumpongeza mkuu huyo wa Wilaya ni kutokana na mambo mbalimbali aliyokwisha yasimamia katika kipindi cha muda mfupi tangu kuteuliwa kwake.
“Tumefurahishwa kwanza na kitendo cha mkuu wa Wilaya kutukusanya wakati wa funga ya waislam, alituita wote bila kujali dini na kwa kauliyake mwenyewe akasema nimeona tufuturu pamoja kwasababu Serikali ya Same haina Dini watu wa Same ndio wenye Dini zao maneno yale yalitubariki sana”. Alisema Mwenyekiti wa Baraza la Wazee.