Baraza la madiwani Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita limeazimia kumfukuza kazi ofisa mtendaji wa kijiji cha Shibumba, Edward Sahani kwa kosa la ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 12.
Mtendaji huyo amefukuzwa kazi baada ya baraza kujigeuza kuwa kamati na kuwajadili baadhi ya watendaji wa serikali wanaoenda kinyume na taratibu za utumishi wa umma na hapa mwenyekiti wa halmashauri hiyo John John anasema.
"Edward Muagala Sahani, aliyekuwa mtendaji wa Kijiji cha Shibumba, baraza limeazimia afukuzwe kazi na vyombo vya kisheria vimchukulie hatua kama raia kwa kosa la ubadhirifu wa fedha za halmashauri kiasi cha shilingi 12,669,639.32 na fedha hizo zirejeshwe kwani ni fedha halali inayodaiwa na halmashauri," amesema.
Aidha baraza hilo limewarejesha kazini watumishi wawili,waliokuwa wamesimamishwa kazi kwa tuhuma ya ubadhirifu wa fedha za Halmashauri.
Licha ya baraza kumwelekeza Mkurugenzi Mtendaji na kumwagiza mweka hazina kuhakikisha wanasiamamia ukusanyaji wa matapo ,lakini halmashauri hiyo imekusanya vyema mapato yake kwa nusu mwaka huu wa fedha.