Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Barabara zinavyokuza maendeleo Lindi

9dcb6845e814e55f9f3b8ce945026964 Barabara zinavyokuza maendeleo Lindi

Tue, 8 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SEKTA muhimu zinazochangia kukua kwa uchumi wa Tanzania ni pamoja na utalii, viwanda, madini na kilimo.

Katika sekta ya kilimo, mazao makuu yanayouzwa nje na kuiingizia nchi fedha za kigeni ni pamoja na tumbaku, pamba, mkonge, korosho, kahawa, chai na karafuu.

Kwa upande wa mkoa wa Lindi ambao makala haya yanaungazia, ni miongoni mwa mikoa inayolima zao la korosho kama zao la biashara kwa wingi pamoja na ufuta.

Lakini Lindi pia husifika kwa kilimo cha nazi mbali na mazao ya chakula kama mhogo, mahindi na viazi.

Kwa upande wa utalii, mkoa huo una maneo mengi ya malikale kama wilaya ya Kilwa, eneo alilopatikana mjusi mkubwa zaidi duniani (Tendeguru), pori la akiba la Selous na kadhalika.

Lakini mkoa wa Lindi pia kuna shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwa ni pamoja na uchakataji wa gesi na viwanda vidogo na vikubwa.

Mkoa huo unapakana na Bahari ya Hindi upande wa Mashariki, Mkoa wa Pwani upande wa Kaskazini, Morogoro na Ruvuma upande wa Magharibi na upande wa Kusini Lindi inapakana na Mtwara.

Takwimu zinazopatikana kwenye tovuti ya mkoa mkoa huo zinaonesha kwamba pato la Lindi limeendelea kuongezeka kutoka shilingi 695,361,000 mwaka 2009 hadi kufikia shilingi 1,690,403,000 mwaka 2015.

Ili pato la mkoa huo wa kusini mwa Tanzania lizidi kukua na uchumi kuimarika, miundombinu bora ya barabara inatajwa kuwa kiungo cha lazima kutokana na umuhimu wake katika kusafirisha mazao ya wakulima pamoja na kusisimua shughuli zingine za kiuchumi ikiwemo utalii.

Hapo ndipo inakuja sababu ya kuishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ambao, kama ilivyo kwa mikoa mingine nchini, umefanya kazi kubwa katika kuboresha barabara za miji na vijiji vya mkoa huo.

Mkulima wa ufuta pamoja na korosho katika kijiji cha Nangurugai katika Halmashauri ya Ruangwa, Juma Hasani, anasema kwa miaka mingi wamekuwa wakipata shida ya kusafirisha mazao yao kutoka kata ya Nangurugai kwenda Ruangwa kuliko na soko la uhakika kutokana na kukosekana kwa daraja katika mto Mbwemkulu.

“Lakini kwa sasa tunawashukuru sana Tarura kwani wameanza kutujengea daraja hilo ambalo litakuwa mkombozi kwa wakazi wa maeneo yetu.

Hili daraja litakuwa ni kiungo kati ya Ruangwa na kijiji chetu,” anasema. Anasema barabara hiyo ni muhimu sana kwao kiuchumi kwa kuwa itarahisisha shughuli zao za kiuchumi kwa kuzingatia kwamba wao ni wazalishaji wakubwa wa korosho na ufuta.

Mkulima huyo anasema barabara hiyo pia inaunganisha Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Liwale. Mpaka kukamilika kwa daraja hilo lenye urefu wa mita 75 gharama zake zinatajwa kuwa ni Sh bilioni 1.6.

Kata ya Mingumbi kuelekea Chapita wilayani Kilwa ni maeneo ambayo yanazalisha nazi kwa wingi. Lakini zamani yalikuwa hayafikiki kirahisi, hasa wakati wa masika kama anavyosimulia, Yusuph Omari.

“Tulikuwa na shida sana sisi wakulima wa nazi, barabara ya Mingumbi – Chapita inayounganisha kata ya Mingumbi kuelekea Chapita na kata ya Namayuni ilikuwa haipitiki kabisa wakati wa masika.

Kwa hiyo shughuli zetu tulikuwa tunafanya wakati wa kiangazi pekee.” Anaendelea: “Lakini tokea hawa wenzetu wa Tarura waanze kusimamia barabara zetu hizi za vijijini, hii barabara inapitika kwenye kipindi chote cha mwaka.”

Kaimu meneja wa Tarura wilayani Kilwa, Ennoc Mshiha anasema barabara hiyo ya Migumbi – Chapita yenye urefu wa kilomita 19.25 wamejinga kwa changarawe na baadhi ya maeneo yasiyo korofi imejengwa kwa udongo. Anataja barabara nyingine walioishughulikia ni ya Mt. Kimwaga – Kandawale yenye urefu wa kilomita 20.

“Hii nayo kabla ya kuanzishwa kwa Tarura ilikuwa haipitiki na hasa kipindi cha mvua. Sisi Tarura kama wenye dhamana ya kuzisimamia barabara hizo tuliamua kuifanyia matengenezo pamoja na kuijengea baadhi ya vivuko ili iweze kupitika kwa mwaka mzima,” anasema.

Anasema barabara hiyo inapita katika maeneo ya wafugaji na hivyo kupitika kwake kunarahisisha usafirishaji mifugo na kupunguza gharama. Ludoviki Chunta, mkazi wa Nachingwea, anazungumzia namna ukarabati wa barabara ya Kilimalondo – Kiegei – Mbwemkuru ilivyoleta chachu kubwa ya maendeleo yao kiuchumi baada ya kujengwa na Tarura.

“Tulikuwa tunapata shida sana katika barabara hii (yenye urefu wa kilomita 26.8) kwani ikifika kipindi cha mvua barabara haipitiki kabisa.

Lakini kwa sasa barabara inapitika muda wote baada ya kufanyiwa matengenezo na Tarura,” anasema.

Chunta anasema barabara hiyo inaunganisha kata tatu zinazolima korosho na ufuta kwa kiwango kikubwa.

Kwa upande wa Manispaa ya Lindi, barabara ya Likabuka – Jangwani yenye urefu wa kilomita 10.3 ambayo ilikuwa inasumbua Menja wa Tarura wa Manispaa hiyo, Marksensius Mwenda anasema barabara hiyo sasa itakuwa inapitika katika vipindi vyote vya mwaka.

“Barabara nyingi zilizokuwa kama zimesahaulika katika Manispaa ya Lindi zimejengwa au kukarabatiwa,” anasema. Anaongeza: “Kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 tulipata shilingi bilioni 7 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za mjini zenye urefu wa kilomita 6.2 kwa kiwango cha lami.

Fedha hizo zilitoka katika mfuko wa kuendeleza miji, yaani mradi wa ULGCP. Hivyo barabara hizo zimesaidia kuboresha sana Manispaa ya Lindi ambapo ndipo makao makuu ya mkoa wa Lindi,” anasema.

Anaongeza: “Maeneo ambayo hayakuwa na taa za barabarani sasa zipo. Kwa kifupi mwananchi ambaye alifika Lindi miaka mitano iliyopita, akifika leo atashuhudia mabadiliko makubwa sana katika sekta ya barabara.”

Anasema wamefanyia pia matengenezo barabara ya Mtutu kuelekea Cheleweni (kilomita 18.3) lakini anasema barabara hiyo bado ina changamoto ya kupitisha maji mengi ya mvua yanayoifanya iharibike mara kwa mara.

“Kwa sasa tumejenga mifereji katika barabara hiyo yenye urefu wa kilomita nne na madaraja madogo madogo 15 pamoja na makalavati makubwa mawili ya boksi, ili kuwawezesha wananchi kupita kwa vipindi vyote vya mwaka hasa kwenye maeneo ya miinuko,” anasema Mwenda Meneja wa Tarura wa Halmashauri ya Lindi kwa maana ya Lindi vijijini, Dausoni Paschal, anasema moja ya mradi wanaoutekeleza ni ujenzi wa daraja la Mnyangala.

“Hili daraja tunalijenga kwa awamu mbili, awamu ya kwanza tumeanza kwa kusimika nguzo, awamu ya pili tutaweka slabu ya juu ya daraja pamoja na ukuta kwa ajili ya kulinda kingo za mto,” anasema.

Ujenzi wa daraja hilo la Mnyangala, anasema linatarajiwa kugharimu Shilingi milioni 450 mpaka kukamilika kwake.

Kwa sasa anasema daraja linaendelea kujengwa katika kata ya Mipingo ambapo katika eneo hilo kuna utalii wa mjusi mkubwa aliyepo Ujerumani (Tendeguru).

Kwa upande wake, Mratibu wa Tarura Mkoa wa Lindi, Agatha Mtwangambale anasema: “Tuna jukumu la kuhakikisha tunasimamia na kuzifanyia matengenezo barabara zote ambazo zipo chini ya wakala wetu ili kuhakikisha zinapitika kwa wakati wote wa vipindi vya mwaka.”

Anasema wanaendelea na utambuzi wa barabara nyingine na kuzifanyia uhakiki na kwamba baada ya muda mfupi, wanatarajia kuongeza mtandao wa barabara, jambo ambalo litazidi kusogeza huduma kwa jamii.

Anasema hakuna halmashauri katika Mkoa wa Lindi ambayo haijanufaika na ujenzi au ukarabati wa barabara tangu wakala huo ulipoanza rasmi kazi takriubani miaka mitatu iliyopita.

Anasema barabara zilizojengwa kwa ahadi za viongozi ni pamoja na barabara ya Stendi Sokoni yenye urefu wa kilomita 1.3, inayozunguka stendi kuelekea katika soko la mji wa Liwale.

Anasema ujenzi wake umegharama shilingi milioni 500. Barabara hiyo anasema ilikuwa ni ahadi za viongozi katika Halmashauri ya Liwale na kwamba ilitolewa na Rais Magufuli mwaka 2015 wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huo.

“Barabara hiyo kwa sasa imekamilika kwa asilimia 100,” anasema. Anaongeza: “Licha ya miradi mingi na mikubwa tunayoitekeleza bado tunakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti, kwa ajili ya kutekeleza matengenezo ya baadhi ya barabara ambazo zinafanya shughuli kubwa za kiuchumi.”

Agatha anazungumzia barabara ya Hotel Tatu – Mkazambo – Pande – Mtandura yenye urefu wa kilomita 36.89 ilioko wilayani Kilwa kwamba ni moja ya barabara zinazosuburu bajeti ili ifanyiwe kazi.

Anasema takribani asilimia 80 ya udongo wa barabara hiyo ni mfinyanzi, hivyo imekuwa changamoto kubwa kwa wananchi katika kuitumia.

Anasema barabara hiyo inapita kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa korosho bora zaidi duniani huku mazao ya samaki kutoka kata ya Mtandura, pamoja na mazao ya mhogo na ufuta yakitegemea pia kupitia katika barabara hiyo.

Mratibu huyo wa Tarura anasema ufinyu wa bajeti pia umesababisha kutotengenzwa kwa ukamilifu wake barabara ya Naiwanga – Nanjirinji yenye urefu wa kilomita 99.72 wilayani Kilwa.

Anasema barabara hiyo ni muhimu kwani Nanjirinji ndio inaongoza mkoani Lindi kwa kilimo cha ufuta na uvunaji wa mazao ya miti kwa maana ya mbao.

Anasema kukamilika kwa barabara hiyo kutaunganisha barabara mbili za mkoa, yaani Barabara ya Nangurukuru – Liwale na Barabara ya Kiranjeranje – Ruangwa.

Chanzo: habarileo.co.tz