Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Barabara za Tanroads zikamilike kabla ya mvua’

0f3f7163c04ac922dbb8cb2504eb1b2a ‘Barabara za Tanroads zikamilike kabla ya mvua’

Wed, 25 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amewataka wakandarasi wote wanaojenga barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Dodoma kukamilisha ujenzi na ukarabati wa barabara hizo kabla ya msimu wa mvua haujaanza.

Alitoa maagizo hayo alipofanya ziara za kushtukiza katika maeneo yenye barabara zilizoharibika na zinafanyiwa marekebisho katika eneo la Makutupora, Mailimbili na kipande cha kilometa nne kilichopo eneo la Mpunguzi jijini humo.

Mahenge aliwaagiza watendaji wa Tanroads kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu na kwenda kwenye maeneo yanayojengwa barabara, lakini pia wanafuatilia taratibu zote zikiwemo za wakandarasi kupewa vibali vya msamaha wa kodi ili kujenga barabara hizo haraka kabla ya msimu wa mvua kuanza kunyesha mkoani humo.

Akizungumza baada ya kukagua barabara ya Makutupora katika kipande cha kilometa moja kinachojengwa na Kampuni ya Sino Hydro ya China iliyoanza kurekebishwa tangu Agosti mwaka huu, Dk Mahenge aliwataka Tanroads kumsimamia mkandarasi huyo na kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa kipande hicho Desemba 31, 2020 kama mkataba wake unavyoonesha.

"Mkandarasi anayejenga kipande cha Makutupora anatakiwa kukamilisha mapema kwa gharama zake kwani kipo ndani ya mkataba wake wa kujenga barabara ya Dodoma hadi Mayamaya kilometa 45 hivi, lakini kiliharibika ndani ya muda wa matazamio kabla ya kukabidhi barabara hiyo rasmi," alisema.

Mkuu wa mkoa huyo aliwataka Tanroads kumfuatilia na kumsimamia kwa karibu mkandrasi wa kipande cha Maili Moja, Kampuni ya Nyanza Construction na kuhakikisha anakamilisha kipande hicho baada ya kukamilisha kazi ya kujenga barabara ya kuzunguka Uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya uapisho wa Rais John Magufuli.

Akizungumza baada ya kukagua kipande cha kilometa nne katika eneo la Mpunguzi, km 30 barabara ya Iringa, Dk Mahenge aliwataka Tanroads kuhakikisha wanafuatilia Wizara ya Fedha na Mipango ili kupata cheti cha msamaha wa kodi ili mkandarasi GNMS Contractors Co. Ltd kuanza ujenzi wa kipande hicho kabla ya mvua.

Kutokana na kukwama kwa vibali vya msamaha wa kodi, Dk Mahenge aliahidi kusaidia kufuatilia wizarani ili kuhakikisha kibali kinatoka mapema ili mkandarasi aanze ukarabati wa kipande hicho haraka na kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa Sh bilioni 2.3 ambayo mkataba wa ujenzi ulisainiwa Septemba 3, mwaka huu.

Mahenge aliwataka Tanroads kusimamia kwa karibu ujenzi wa barabara mbalimbali mkoani humo ikiwemo ya Mpwapwa kutoka Kongwa, Mvumi, Bihawana na Mrijo ambazo zote zinatakiwa kukaguliwa ili kuona kama makandarasi wanaendelea na kazi.

Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dodoma, Salome Kaganda alisema aliahidi kuwafuatilia wakandarasi waliopewa barabara mbalimbali kukamilisha ndani ya mkataba.

Chanzo: habarileo.co.tz