Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Barabara ya mzunguko Ubungo yapunguza foleni

48891 Pic+barabara

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Suluhisho la foleni kubwa ambayo imedumu muda mrefu katika makutano ya barabara za Morogoro, Nelson Mandela na Sam Nujoma Ubungo jijini Dar es Salaam limeanza baada ya ujenzi wa barabara za juu kuanza.

Licha ya makutano hayo kuwa na taa za kuongozea magari, iliwalazimu askari wa usalama barabarani kuingilia kati asubuhi na jioni ili kupunguza foleni kubwa iliyokuwa kero kwa watumiaji.

Hata hivyo, wakati ujenzi huo ukiendelea hali ni tofauti baada ya kutengenezwa mzunguko ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza foleni katika eneo hilo ambalo lilionekana kuwa kero kutokana na foleni.

Kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi wa barabara hizo za juu, zinatarajiwa kukamilika Desemba mwakani.

Watumiaji wa barabara hiyo walisema foleni hiyo ilikuwa kero kwa kipindi kirefu kabla ya ujenzi huo kuanza jambo lililosababisha watumie muda mrefu kuvuka eneo hilo.

Wakizungumza na Mwananchi juzi, walisema hivi sasa barabara hiyo imepungua foleni wakati huu ujenzi wa barabara za juu ukiwa umeshika kasi.

“Sasa ni raha kupita eneo la Ubungo mataa hakuna foleni asubuhi wala jioni na hatupiti tena barabara ya Ubungo maziwa kukwepa foleni. Yaani kuna muda nawaza kwa nini hiki kitu hawajakibuni tangu mwanzo,” alisema Ally Idarous dereva wa daladala linalofanya safari zake Segerea na Makumbusho.

Naye Alfred Mulolo mwenye daladala linalofanya safari zake kati ya Mbagala na Simu 2000, alisema mzunguko huo umewasaidia kuepuka foleni iliyokuwa kero na sasa wanatumia dakika 20 hadi 25 kutoka Buguruni hadi kuvuka eneo hilo. “Kabla ya mzunguko nilikuwa nikifika eneo hili (Ubungo mataa) nakata tamaa maana mafuta yalikuwa yanaishia njiani hakuna faida inayopatikana,” alisema Mulolo.

Dereva wa gari ndogo Boniface Michael alisema amekuwa akitumia barabara hiyo na humchukua nusu saa hadi dakika 45 kwenye foleni, lakini sasa hata dakika tano haziishi anavuka kutokea Mwenge kwenda Tazara kutokana na mzunguko uliojengwa na mkandarasi.



Chanzo: mwananchi.co.tz