Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Barabara vijijini kuundiwa mfuko

D1112aacc5c41513d1ef5ce85006be63 Barabara vijijini kuundiwa mfuko

Fri, 25 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema serikali itaanzisha Mfuko wa Barabara Vijijini utakaotumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA).

Dk Mwigulu ametoa msimamo huo bungeni Dodoma wakati wa kujibu hoja za wabunge waliochangia Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2021. Muswada huo umepitishwa.

Wabunge waliishauri serikali iweke utaratibu ili fedha za TARURA ziende moja kwa moja kwa wakala huo hasa kwa kuwa serikali imerekebisha Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220.

Wabunge walisema Mfuko wa Barabara Vijijiji utaongeza uwezo wa TARURA wa kuimarisha miundombinu ya barabara na hivyo kuchochea uchumi.

“Kwa hiyo tumekubaliana na mapendekezo ya kuanzisha mfuko rasimi wa TARURA na wataalamu waharakishe katika hili na kuainisha vyanzo vyote vitakavyoingizwa kwenye mfuko.”

Dk Mwigulu alisema vyanzo vya fedha kwa mfuko utakaoanzishwa ni Sh 100 iliyoongezwa kwenye tozo ya mafuta ya aina yote, asilimia 30 ya mgawo wa fedha za Mfuko wa Barabara na vyanzo vingine vikivyobainisha kuwa ni vya TARURA.

Awali, akichangia muswada huo, Mbunge wa Kalembo, Josephat Kandege aliishauri serikali iongeze kifungu kwenye sheria iliyoanzisha Mfuko wa Barabara ambacho kitahakikisha fedha zilizotengwa au kuelekezwa TARURA zinafika na kutumiwa na wakala huyo.

Mbunge wa Nzega Vijijini, Hamis Kigwangala (CCM) alishauri uanzishaji wa Mfuko wa Barabara Vijijini ili fedha zote ambazo serikali imezitafuta ziingie moja kwa moja kwenye mfuko huo.

Mbunge wa Kibiti, Twaha Mpembenwe (CCM) alishauri fedha zinazotokana na ongezeko la tozo za mafuta zilizoelekezwa kwenye tozo za mafuta kwenda TARURA zikingwe kisheria na kuwa kinyume chake haitakuwa na tija.

Pia ameshauri kanuni zitakazotungwa baada ya mabadiliko ya Sheria zipelekwe kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria kabla ya kuanza kutumika ili kuondoa matatizo aliyoyafananisha na suala la kikokotoo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz