Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Barabara kiwango cha lami kujengwa Nyasa

Mndeme  1024x576 Barabara kiwango cha lami kujengwa Nyasa

Tue, 19 May 2020 Chanzo: --

SERIKALI inatarajia kuunganisha kwa mtandao wa lami mwambao mwa ziwa Nyasa mkoani Ruvuma kuanzia Lituhi hadi Chiwindi mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 129 za ujenzi wa lami nzito yenye urefu wa kilometa 66 toka Mbinga hadi Mbambabay Makao Makuu ya Wilaya ya Nyasa ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 50.

Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Mtupale wilayani Nyasa, Mndeme amesema katika bajeti ya mwaka huu serikali imeingiza kwenye bajeti barabara yenye urefu wa kilometa 41 kuanzia Nang’ombo hadi Chiwindi mpakani na nchi ya Msumbiji.

“Katika mwaka huu tumeweka kwenye bajeti ya fedha barabara hii ifanyiwe usanifu na upembuzi yakinifu ili ijengwe kwa kiwango cha lami’’amesema Mndeme.

Ametoa rai kwa wananchi wakiona watalaam wa barabara wanafika kupima kutoa ushirikiano na kwamba ukarabati unaofanyika kwenye madaraja katika barabara hiyo ni kuwezesha magari kupita katika kipindi hiki cha mpito.

Amesema usanifu na upembuzi yakinifu katika barabara ya Kitai,Lituhi hadi Mbambabay umekamilika na kwamba kinachosubiriwa ni kutenga bajeti ili ujenzi wa barabara uweze kuanza hali ambayo itawezesha wilaya ya Nyasa kuunganishwa na mtandao wa lami.

Mndeme ameongeza kuwa serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha kuwa wananchi wa Nyasa wanaepukana na changamoto ya usafiri na usaifirishaji ambapo tayari serikali imenunua meli tatu ,mbili za mizigo na moja ya abiria na kwamba wakazi wa Nyasa ndiyo watakaonufaika zaidi ya usafiri wa meli hizo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama amewataka wananchi wa Kata ya Chiwanda wilayani Nyasa waliopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji kulinda Nchi ya Tanzania kwa niaba ya Watanzania wengine ili kuhakikisha nchi inakuwa salama kutokana na kwamba serikali itajenga barabara hiyo ili kuimarisha usalama.

Kuunganishwa kwa mtandao wa lami katika wilaya ya Nyasa kutaufanya Mkoa wa Ruvuma kuunganishwa kwa barabara ya lami katika ukanda wa Mtwara korido kuanzia Mtwara hadi Mbambabay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

Chanzo: --