Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Barabara bora zinavyoibadilisha Ruvuma

D4bc059c889971c426cc75eb0ed768df Barabara bora zinavyoibadilisha Ruvuma

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIKA miaka mitano iliyopita, Tanzania imepata mafanikio makubwa kiuchumi kutokana na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.

Uchumi umeendelea kukua kwa kasi ya wastani wa asilimia 6.9 kwa miaka mitano iliyopita, ikiwa ni ukuaji mkubwa zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita na hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi.

Ni kutokana na ukuaji huo, Benki ya Dunia iliitangaza Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati mwaka 2020.

Tathmini iliyofanywa na Benki ya Dunia Julai 2020 juu ya mwenendo wa uchumi wa nchi zote duniani, ilionesha kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa katika kukuza uchumi wake na hivyo kutimiza vigezo vilivyowekwa kwa nchi kuingia katika aina hiyo ya uchumi.

Mambo mengi yamechangia katika kuifikisha hapo Tanzania ikiwemo sekta ya kilimo kinachoajiri Watanzania wengi zaidi.

Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba uzalishaji wa mazao ya chakula uliongezeka kutoka tani 15,528,820 mwaka 2015/16 hadi tani 16,891,974 mwaka 2018/19 wakati mazao ya biashara, uzalishaji pia uliongezeka kutoka tani 796,502 mwaka 2015/16 hadi tani 1,144,163 mwaka 2018/19.

Katika Mkoa wa Ruvuma ambao makala haya yanauangazia, takwimu zinaonesha katika msimu wa mwaka 2015/2016 mkoa ulilima hekta 231,936.6 za mahindi zilizotoa tani 736,692.8 za mavuno lakini katika msimu wa mwaka 2019/2020 Ruvuma ililima hekta 268,008 zilizotoa tani 787,321, za mavuno, sawa na ongezeko la tani 50,628.

Katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2015 - 2020 mkoa umeweza kuzalisha tani 8,547,816 za mazao hadi kufikia mwaka 2020 na hivyo kuufanya mkoa wa Ruvuma kushika nafasi ya nne kitaifa kwa uzalishaji wa nazao ya kilimo.

Mbali na mahindi mazao mengine ya biashara yaliyozalishwa Ruvuma ni maharage, korosho na kahawa.

Kitu kimoja ambacho kimesaidia sana kunyanyua kilimo na hivyo kuchangia kuiharakisha Tanzania kwenye uchumi wa kati, siyo Ruvuma pekee bali Tanzania nzima, ni kazi kubwa iliyofanywa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) katika ujenzi wa barabara na hivyo kusaidia wakulima kufikisha haraka mazao yao sokoni.

Kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma, Tarura imekuwa na mpango kazi wa kuhakikisha miundombinu bora ya barabara, hasa mashambani, inapitika na hivyo kurahisisha usafirishaji wa mazao hayo kwa haraka na kwa gharama nafuu.

Wilfred Mwanga, mkulima wa zao la maharage katika Halmashauri ya Madaba, Kata ya Wino, anasema katika kata yao wanalima sana mazao ya maharage, mahindi, ndizi, mpunga, tangawizi pamoja na uvunaji wa mazao ya misitu.

Vilevile katika kata hizo anasema kunaendeshwa shughuli za kijamii kama vile shule na vituo vya afya na hivyo mahitaji ya miundombinu ya barabara bora na za uhakika yalikuwa muhimu sana.

Mwanga anashukuru ujio wa Tarura katika serikali ya awamu ya tano ambao umesaidia sana ujenzi wa barabara ambazo zilikuwa zimeshindikana kupitika kwa mwaka wote lakini sasa wanapita bila matatizo.

“Kabla ya kutengenezwa kwa barabara hizi katika kata yetu ya Wino tulipata changamoto kubwa ya kufikisha mazao yetu kwenye soko au wateja wa mazao yetu kuja huku kwetu. Lakini kwa sasa tunaishukuru sana Tarura kwa kututengenezea barabara,” anasema Mwanga.

Barabara anayoizungumzia ambayo kwao imekuwa mkombozi ni ya Wino – Ifinga – Luhuiji, yenye urefu wa kilomita 48 iliyotengenezwa kwa kiwango cha changarawe pamoja na udongo.

Barabara hiyo muhimu, hainufaishi wakazi wa kata ya Wino pekee bali pia kata za Ifunga na Lohuji na imejengwa katika mwaka wa fedha wa 2020/2021.

Mkulima wa mpunga katika kata ya Namtumbo, Adamu Ngonyani, anaishukuru pia serikali ya awamu ya tano kwa kuwatengenezea barabara ya Ligera – Jiungeni ambayo inaunganisha kijiji cha Ligera na kuelekea katika kijiji cha Jiungeni. Barabara hiyo iliyojengwa na Tarura ina urefu wa kilomita 17.4.

“Kabla ya ujenzi wa hii barabara, tulipata shida sana katika kusafirisha mazao yetu lakini Tarura wametuondolea hilo tatizo kwa kututengenezea barabara hii ikiwa ni pamoja na kutujengea madaraja matatu pamoja na mifereji ya zege ili kuweza kupitisha maji ya mvua,” anasema.

Anasema barabara hiyo ni muhimu sana kwa wakazi wa Ligera na Jiunge ambao ni wazalishaji wakubwa wa zao la mpunga.

Mwingine anayemimina kongole kwa Tarura ni Kostantine Komba, mkazi wa kijiji cha Lundo. Hilo linatokana na maelezo yake kwamba hapo awali wananchi na wakazi wa eneo hilo walipata sana shida ya kuvuka Mto Lumeme kutokana na kukosa daraja la uhakika.

Komba anasema katika kumbukumbuku zake, takribani watu wanane wameliwa na mamba ndani ya muda mfupi katika mto huo wakiwa katika harakati za kuvuka kwenda ng’ambo nyingine.

Anasema anawashukuru Tarura kwa kujenga madaraja matano kwa ajili ya vivuko vya watu ambao wengi wao ni wakulima wakubwa wa zao la mpunga na wanafunzi waliokuwa wanakwenda shule kujipatia elimu.

Anasema barabara inayopita katika mto huo ambayo pia imejengwa inaunganisha wilaya ya Nyasa na Halmashauri ya Mbinga vijijini.

“Hii barabara inatupunguzia umbali mrefu sisi wananchi ambao tulikuwa tunalazimika kuzunguka umbali mrefu kwenda Mbinga,” anasema.

Meneja wa Tarura wa Wilaya ya Nyasa, Tomath Kitusi anasema, moja ya changamoto waliyonayo sasa kukosekana kwa daraja muhimu katika kata ya Kilosa. Anasema baada ya kunyesha kwa mvua nyingi, daraja hilo lilisombwa na maji ya mvua.

Anasema awali daraja hilo lilikuwa na upana wa mita 30, lakini baada ya kunyesha kwa mvua nyingi mwaka huu kingo zimeharibika hadi kufikia mita 120.

Anasema eneo hilo ni muhimu kwani kuna uwekezaji wa machimbo ya makaa ya mawe.

Mmoja wa wawekezaji hao wa kuzalisha makaa ya mawe ni Gody Mwanga ambaye sasa analazimika kuzunguka umbali mrefu huku njia husika ikiwa pia na changamoto ya milima kabla ya kuifikia barabara kubwa.

Meneja wa Tarura katika Halmashauri ya Songea, John Ambrose anasema katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 wanafanyia matengenezo barabara ya Kiheo – Liura, yenye urefu wa kilomita sita huku kilomita 1.5 zikiwa hazijafunguliwa.

Anasema katika mwaka huu wa fedha wa 2020/2021 wamemwaga zege kwenye mlima Kiheo katika kipande cha urefu wa mita 600.

Anasema hatua hiyo inawasaidia wananchi kupitia njia inayokatiza kwenye mlima Kiheo ambayo ni nyepesi wakati wanaftafuta mahitaji yao ya msingi katika mji wa Songea.

Chanzo: habarileo.co.tz