Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari ya Tanga yapokea meli kubwa

1726ae0b5c408e8cf1cd600684a79da1 Bandari ya Tanga yapokea meli kubwa

Sat, 28 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MELI kubwa ya mizigo yenye tani 55,000 imetia nanga katika bandari ya Tanga baada ya kukamilika kwa uongezwaji wa kina katika eneo la gati awamu ya kwanza uliogharimu takribani Sh bilioni 256.

Tukio hilo linalotajwa kuwa ni kubwa na la kujivunia, limekuja ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli wakati wa ziara yake akiitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuongeza kina katika bandari kuruhusu meli kubwa kutia nanga karibu na bandarini.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa meli ikitia nanga bandarini jana, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela alisema huo ni ushahidi tosha wa namna serikali ilivyojikita kuboresha uchumi katika sekta mbalimbali. Shigela alisema uamuzi wa Rais Magufuli ni wa kutaka meli kubwa zitie nanga bandarini hapo kwa wingi ili Mkoa wa Tanga pia utoe mchango katika uchumi wa nchi.

“Ningeiomba Bodi ya TPA kupunguza tozo ambazo ni kero ili sasa kuweza kusaidia wakazi wa Tanga na nchi jirani waweze kutumia bandari hii na kuachana utaratibu wa sasa kushusha mizigo katika bandari iliyoko nchi jirani ya Kenya,” alisema mkuu wa mkoa. Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Donald Ngaile alisema awali serikali ilikuwa ikitumia gharama kubwa katika kushusha na kupakia mizigo katika umbali wa kilometa 1.7 baharini.

Ngaile alisema baada ya upanuzi wa kina, meli kubwa zinaweza kutia nanga karibu na hivyo kusaidia kumpunguzia mteja adha aliyokuwa akiipata hapo awali. “Tulikuwa tunalazimika kufanya ‘double handling’ (upakuaji na upakiaji mara mbili) za mizigo katika kupakia na kupakua shehena ya mizigo jambo ambalo lilikuwa linatuongezea gharama za uendeshaji, lakini baada ya maboresho yaliyofanyika gharama zitapungua,” alisema Ngaile.

Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu alisema kufanya vizuri kwa bandari hiyo ni kufanya vizuri kwa uchumi wa wanatanga na taifa kwa ujumla.

Alisema aliomba ridhaa ya kugombea jimbo hilo ili kuwatumia wananchi wa Tanga kuwaletea maendeleo. “Tuliwaahidi wakati wa kuomba kura kuwa iwapo Serikali ya CCM itaingia madarakani kipaumbele chake ni maendeleo kwa wananchi kama haya tunayoyashuhudia leo,” alisema Ummy.

Chanzo: habarileo.co.tz