Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari ya Kagunga yaanza kutoa huduma

55a1d0392e092948adea3492d5173ee3 Bandari ya Kagunga yaanza kutoa huduma

Fri, 8 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imetangaza kuanza kutoa huduma katika Bandari ya Kagunga iliyopo wilaya ya Kigoma, mwambao wa Kaskazini wa Ziwa Tanganyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa Desemba mwaka jana akitaka bandari hiyo ianze kazi Januari Mosi 2021.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko akizungumza mbele ya Mkuu wa mkoa Kigoma alipotembelea na kukagua utekelezaji wa maagizo hayo ya Waziri Mkuu alisema kuwa bandari hiyo imeanza kutoa huduma huku baadhi ya mapungufu ya kiutendaji yakiendelea kufanyiwa maboresho.

Kakonko alisema kuwa ujenzi wa bandari hiyo uliogharimu kiasi cha Sh Bilioni 3.8 ulikamilika mwaka 2017 lakini bandari ilishindwa kutoa huduma kutokana na changamoto mbalimbali na kwamba pamoja na changamoto hizo utoaji huduma utaanza na changamoto zilizopo zitaendelea kufanyiwa kazi.

Alisema kuwa ili kuhakikisha bandari inafanya kazi kwa tija na meli kutia nanga kwenye bandari hiyo ameiomba serikali ya mkoa kuweka utaratibu wa kuhakikisha meli zote zinazotoka nje ya nchi au zinazokwenda nje ya nchi zinapitia bandarini hapo kwa ajili ya kupata kibali cha kuingia na kutoka nchini.

Sambamba na kuanza kazi kwa utoaji huduma kwa bandari ya Kagunga iliyopo mpakani mwa Tanzania na Burundi pia TPA ilikabidhi jengo la soko kwa Halmashauri ya wilaya Kigoma lililojengwa kwa thamani ya shilingi milioni 300 na majengo ya kituo cha polisi ambayo pia yamejengwa na TPA.

Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa wilaya ya Buhigwe, Michael Ngayarina alisema kuwa kuanza kwa utoaji huduma wa bandari hiyo siyo tu muhimu kwa shughuli za uchumi na biashara kwa mkoa lakini pia linaongeza usimamizi wa masuala ya ulinzi na usalama kwa eneo hilo.

Andengenye alisema kuwa serikali ya mkoa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazopaswa kutoa huduma kwenye bandari hiyo watafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba utoaji huduma katika bandari hiyo unakuja na tija kwa wananchi kiuchumi na kiusalama.

Makamu Mwennyekiti wa bodi ya TPA, Dk Delphine Magere alisema kuwa bodi ilipokea maelekezo ya Waziri Mkuu na kutoa maagizo kwa menejimenti ya kuyafanyia kazi na kwamba kuanza kazi kwa bandari hiyo kunalenga kuleta faida kiuchumi kwa serikali na wananchi huku akitaka wananchi wa eneo hilo kuhakikisha wanalinda na kutunza miundombinu ya bandari hiyo.

Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Asa Makanika akizungumza wakati wa kukagua utekelezaji wa agizo hilo alisema kuwa pamoja na bandari kuanza kazi ameiomba serikali kuangalia utekelezaji wa kupeleka barabara katika bandari hiyo kutokea mjini Kigoma yenye urefu wa kilometa 60 ili kuondoa adha ya watu wanaotaka kwenda kwenye bandari kuzungukia nchi jirani ya Burundi.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoa Kigoma, Jacob Mtemang'ombe alisema kuwa bado eneo hilo lina changamoto ya kutokuwepo kwa umeme na mtandao wa intaneti kuruhusu shughuli za mamlaka hiyo kufanyika kimtandao lakini alibainisha kuwa wameshapeleka watumishi ambao watakuwepo kwenye eneo hilo kutoa huduma ambazo TRA inapaswa kutoa.

Chanzo: habarileo.co.tz