Kigoma: Jumla ya Sh930 milioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika Bandari ya Kagunga mpakani mwa Burundi na Tanzania kwa kiwango cha changarawe.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 10, 2019, Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese amesema fedha hizo zinajumuisha ulipaji fidia kwa wananchi kupisha ujenzi.
Kaimu mhandisi wa TPA, Nyakato Namnana amesema pamoja na ujenzi wa barabara katika Bandari ya Kagunga, kutakuwa na ujenzi wa soko la kisasa litakalowanufaisha wafanyabiashara watakaokuwa wanatumia bandari hiyo wakiwamo wa DR Congo na Burundi.
Katika kuboresha shughuli za bandari, tayari wamekamilisha ujenzi wa gati ambalo limegharimu zaidi Sh3 bilioni lenye uwezo wa kubeba mzigo tani 6,000 kwa wakati mmoja. Ujenzi wa Bandari wa Kagunga unajumuisha majengo ya ofisi, abiria na nyumba za askari.