Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari Kigoma muhimu Burundi, DRC

5896 Nditiye TZW

Fri, 6 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imesema ni kweli katika mkutano wa mawaziri wa uchukuzi wa Uganda, Burundi, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Tanzania waliazimia kuwa, kuanzia Januari mwaka huu bandari ya Kigoma iwe ya mwisho kwa bidhaa za Burundi na mashariki ya DRC.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandishi Atashasta Nditiye amesema bungeni mjini Dodoma kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa bandari hiyo kwa uchumi na ustawi wa Kigoma na inategemewa na wananchi kwenye mkoa huo na mikoa jirani.

Ameyasema hayo wakati anajibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto kwenye kikao cha tatu cha Mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Tanzania.

Mhandisi Nditiye amesema, bandari hiyo pia ni muhimu katika utoaji wa huduma ya usafirishaji wa bidhaa zinazopitia reli ya kati kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani za Burundi na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa gharama nafuu.

Amewaeleza wabunge kuwa, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga fedha kuendeleza bandari ndogo za Ujiji na Kibirizi ili ziweshe miradi kama vile Ujiji City.

Amesema, zabuni kwa ajili ya kuendeleza bandari hizo zimefunguliwa Aprili tatu mwaka huu na jumla ya kampuni 21 zimeonesha nia ya kufanya kazi hizo.

Zabuni kumpata mkandarasi wa ujenzi wa bandari hizo ilitangazwa awali lakini hakuna mzabuni hata mmoja aliyejitokeza kuomba kazi hizo.

Chanzo: habarileo.co.tz