Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Balozi Mushi awashangaa wanaoponda uteuzi wa Jokate

13325 Jokate+pic TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa idara ya kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Celestine Mushi amesema wanawake wanapoteuliwa kushika nafasi mbalimbali za kisiasa na serikalini nchini, wamekuwa wakishambuliwa.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 23, 2018  katika mkutano wa Jinsia na Habari ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Mushi ametoa mfano uteuzi wa mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, kubainisha kuwa wapo waliokosoa uteuzi huo.

“Kwanza tulitakiwa kumpongeza rais kwa kumteua msichana mdogo kushika nafasi hiyo na baada ya hapo tumuhukumu  Jokate kwa kazi yake atakayofanya,"amesema.

Amesema jamii haitakiwi kurekebisha mabaya kwa kuibua mabaya bali kutafuta njia nzuri ya kutatua yaliyo mabaya.

Amebainisha kuwa mitandao ya kijamii inatakiwa kutumika vyema na wananchi na si vinginevyo, ikiwa ni pamoja na kudhalilisha na kuvitaka vyombo vya habari kuwasaidia vijana kuendana na sayansi na teknolojia ili wasiathirike.

Akizungumzia mitandao ya kijamii mkurugenzi wa  kitengo cha wanawake wa UN, Dk Phumzile  Mlambo-Ngcuka amesema, “unachotuma leo kwenye mitandao ya kijamii kinaweza kukuathiri kesho."

Amesema vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii vinatumika kumkandamiza mwanamke.

"Kama mwandishi atatumia juhudi zake kuhakikisha mwanamke anapata nafasi katika habari na kuepuka kumuandika katika mtazamo hasi hili tatizo litakwisha,"amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz