Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Balaa linalokuja kwa wamiliki wa gereji Dar es salaam

Gereji (1000 X 562) Balaa linalokuja kwa wamiliki wa gereji Dar es salaam

Fri, 15 Oct 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jiji la Dar es Salaam kama yalivyo maeneo mbalimbali nchini lina sifa zake za kipekee, ikiwamo ya uwepo wa gereji nyingi zilizoanzishwa kwenye maeneo ya makazi.

Gereji hizi maarufu kama ‘gereji bubu’ zimetamalaki katika maeneo kama vile Tandale, Temeke, Mwananyamala na mengineyo. Uwepo wake unakosolewa na watu wengi wanaosema gereji hizo zimekuwa kero kwa wananchi kwa sababu ya kuzalisha takataka, kuziba njia kwa watumiaji wa barabara na hata kuathiri afya za wananchgi jirani na gereji hizo.

Hali hiyo imeulazimu uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza kuwaondoa wenye gereji hizo, mkakati unaokwenda sambamba na ule wa kuwaondoa machinga wanaofanya shughuli zao katika hifadhi za barabara na maeneo yasiyoruhusiwa.

Akizungumza na wananchi wa jimbo la Kinondoni Septemba 20, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alisema gereji bubu kwenye maeneo ya hifadhi za barabara, zimekuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira, huku akiwaagiza wahusika kuondoka kabla shughuli ya kuwaondoa haijaanza.

Alipoulizwa kwa simu kufafanua suala hilo, RC Makalla alisema baada ya kuwaondoa wamachinga kitakachofuata ni usafi, kwa kuondoa wenye gereji bubu.

Kuhusu kuwatafutia maeneo mbadala kama ilivyo kwa wamachinga, alisema hilo haliwezekani, kwani baada ya kuwapanga wamachinga, jiji litakachofanya ni kuweka maeneo hayo katika hali ya usafi.

“Hawa hatuna haja ya kuwapanga, mtu ana gari lake atafute nafasi ya kulipeleka, siwezi kumtafutia mtu sehemu ya kulipeleka.Kuna magari mengi binafsi kwenye maeneo ya hifadhi za barabara, huwezi kusema niwatafutie maeneo, hilo haliwezekani wanapaswa waanze kutafuta maeneo mengine,” alisema Makalla.

Hali ilivyo

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini wapo mafundi na wamiliki walioanzisha gereji maeneo yasiyoruhusiwa ikiwemo kwenye hifdhi za barabara, viwanja vya michezo na wengine kudirki kufunga mitaa na kusababisha usumbufu.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wamiliki na mafundi katika gereji hizo walidai endapo watatafutiwa maeneo rasmi na ya kudumu, wako tayari kuondoka.

Rashid Kombo anayetengenezea magari pembezoni mwa barabara ya Magomeni na Sinza alisema, chanzo cha kufanyia shughuli zao katika eneo hilo, ni kutokana na eneo walilokuwepo mwanzo kuondoka ili kupisha ujenzi wa shule.

Alieleza kuwa baada ya kupisha eneo hilo kwa ahadi ya kutafutiwa maeneo mengine, hadi shule imejengwa hawakuwahi kuonyeshwa eneo lingine, hivyo kusababisha baadhi yao kuhamia kandokando ya barabara.

“Mbunge wa wakati huo Idd Azzan aliahidi kututafutia maeneo mengine, lakini hadi anatoka madarakani hakuwahi kukamilisha. Tumebaki maeneo haya kutokana na mazingira ya upatikanaji wa maeneo kuwa magumu,” alisema Kombo.

Aliongeza: “Hatupingi kuondoka ila tunaiomba Serikali itutafutie eneo, na hiki ndio kilio chetu kikubwa kwa muda mrefu, endapo tutapatiwa eneo hata likiwa la mkopo tutalipa kwa kuwa kilio chetu kikubwa ni maeneo rasmi,” alisema.

Naye Abdallah Mdugi anayetengeneza magari eneo la Magomeni Ndugumbi alisema, wamekuwa wakifanya kazi katika eneo hilo kwa amri ya Manispaa pamoja na kufuata sheria zote ikiwemo ulipaji wa ushuru.

Aliongeza kuwa malalamiko yao ni ya muda mrefu, ambayo yalishawasilishwa kwenye ofisi mbalimbali ikiwamo serikali ya mtaa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili waweze kupatiwa maeneo rasmi kwa ajili ya kufanyia shughuli zao.

“Majibu tuliyopewa tulielezwa wakati tunasubiri kutafutiwa maeneo rasmi, tuendelee kufanya shughuli zetu hapa, na sisi tuko hapa kwa amri ya Serikali na kila mwaka tumekuwa tukilipia ushuru,” alisema Mdugi.

Alibainisha kuwa pamoja na kutakiwa kuondoka katika eneo hilo, zipo athari mbalimbali watakazozipata ikiwemo kupoteza wateja.

Serikali za mitaa

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mtogole jijini Dar es Salaam, Hamisa Mpapai alisema, kauli ya Mkuu wa mkoa kuhusu wenye gereji bubu na wanaoegesha magari kando ya barabara, imekuja wakati mwafaka, kwa kuwa kiuhalisia huo ni uchafuzi wa mazingira.

Alisema athari zake ni kubwa kwa jamii, kwani wakati mwingine gereji hizi huwa chanzo cha kulundikana kwa takataka mbaya zaidi, huku maeneo hayo yakiwa hayafanyiwi usafi.

“Mara nyingi tumekuwa tukiwaelekeza wahusika lakini wamekuwa wabishi, wengine wamekuwa wakituelewa lakini wengi wao wamekuwa wakaidi,” alisema Mpapai.

Alisema wakati mwingine gereji hizo zimekuwa kero, kutokana na kuwapo katikati ya makazi ya watu, kuzuia njia na kelele.

Wananchi waeleza kero

Baadhi ya wananchi akiwamo Agatha Francis mkazi wa Manzese, walieleza kukerwa na uwepo wa gereji bubu katikai ya makazi ya watu.

Alisema gereji bubu na biashara ya vyuma chakavu imegeuka kero katikati ya makazi ya watu, kutokana na utaratibu mbovu wanaotumia kufanya shughuli zao.

“Mafundi hawa wamekuwa wakiziba njia, wakati mwingine hata unapokuwa na mgonjwa inakuwa vigumu kupita ili kumwahisha hospitali.

“Kuna wakati wanaziba njia kabisa kutokana na mpangilio wao mbovu, hata ukiwa na mgeni muda mwingine anakosa mahali pa kuegesha gari. Lakini kero nyingine ni uchafu, alisema Agatha.

Mwalimu wa shule ya sekondari Turiani ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alieleza namna gereji hizo zinavyoathiri utulivu hasa wakati wa ufundishaji.

Alibainisha kuwa wakati mwingine mafundi hao hupiga kelele hasa pale wanaponyoosha gari iliyopata ajali au kupuliza rangi.

Kauli ya Jiji la Dar es Salaam

Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri alisema, gereji hazitakiwi kuwepo katikati ya mji na utaratibu wa kuwahamisha ulishafanyika muda mrefu, na kwamba hao waliopo wanakiuka utaratibu.

“Hao wanaosema hakuna maeneo ni waongo, wenzao tuliowahamisha kutoka katikati ya mji tuliwatafutia maeneo Tabata, na hata hawa tukiwaondoa wanapaswa kwenda huko hadi hapo tutakapotafuta maeneo mengine,” alisema Shauri.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Samuel Gwamaka, alifafanua kuwa masuala yote yanayohusu gereji huratibiwa na halmashauri husika, ikiwa ni pamoja na utoaji wa vibali, wanachofuatilia wao ni utunzwaji wa mazingira.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live