Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijjni na Mijini TARURA imeongeza bajeti ya fedha kwaajili ya kuboresha miundombinu kwa Mkoa wa Kagera kutoka Bilioni 9 hadi bilioni 52.3.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya usanifu wa miradi ya uboreshaji miundombinu ya miji Tanzania (TACTIC) kwa miji 15 ya kundi la pili (Tier 2) iliyofannyika tarehe 15 Disember ,2023 katika Manispaa ya bukoba.
“Serikali itaendelea kuleta fedha kuboresha barabara katika eneo letu la Bukoba ukiacha fedha hizi za miradi,fedha tulizokuwa tukileta ilikua ni Bilioni 9 tu lakini kwa sasa kiwango cha fedha tunazoleta ni Bilioni 52.3, nani kama Samia,” aliongeza.
Hata hivyo alisema kupitia mradi huo barabara zaidi ya Km 7 zitajengwa lakini TARURA bado itaendelea kupeleka fedha kwa ajili ya kuboresha barabara .
“Huu ndio msingi wa Tanzania ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, anakwenda kuboresha miundombinu ya mto Kanoni wote kwa kujenga kingo na kuondoa madhara ya mafuriko ili kuwa na mto bora , mzuri ambao utakua na manufaa kwa watanzaniai wanaoishi hapa .
Pia Waziri huyo ame watahadharisha Viongozi wa kisiasa na Serikali kuhakikisha hawakwamishi miradi hiyo na kwamba hatoacha kuchukua hatua dhidi yao.
Naye, Mratibu wa Miradi ya Ushirikiano na Benki ya Dunia kutoka TARURA Mhandisi Humphrey Kanyenye alisema mkataba wa usanifu wa miradi katika miji 15 ya kundi la pili la utekelezaji wa miradi ya uboreshaji miundombinu ya miji ya Tanzania itagharimu takribani shilingi bilioni 8.25 kwa miji yote 15 ya awamu ya pili.
Jumla ya mikataba mitano ilisainiwa kwa kanda kwa mgawanyo wa miji ya Tanga, Korongwe na Moshi,Babati, Singida na Shinyanga, Bukoba, Musoma na Bariadi, Kibaha,Lindi na Mtwara pamoja na kanda ya Iringa, Njombe na Mpanda.
Mhandisi Kanyenye alisema kua Manispaa ya Bukoba imetengewa bajeti ya Bilioni 23 na Miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja ujenzi wa stendi mpya ya kisasa, soko la kisasa mjini kati, ujenzi wa kingo ya Mto Kanoni(Km. 7.3), ujenzi wa barabara za lami(Km 7) na kufunga taa za barabarani kwa barabara zilizokamilika ambazo hazina taa.