Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bajaji zateka soko la daladala, taxi Moshi

89965 Bajaj+pic Bajaji zateka soko la daladala, taxi Moshi

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Usafiri wa pikipiki za magurudumu matatu, maarufu kwa jina la Bajaji, umeanza kuwa tishio la kibiashara kwa waendesha bodaboda, taxi na mabasi madogo ya daladala, maarufu kwa jina la Hiace.

Bajaji sasa zimekuwa kimbilio la wengi katika mji wa Moshi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa kuwahoji wadau, unaonyesha baadhi ya abiria hawataki tena kutumia usafiri wa bodaboda kutokana rekodi mbaya ya ajali inayosababisha vifo na ulemavu.

Kutokana Bajaji kuteka soko, kumeibuka misuguano kati ya madereva na makondakta wa daladala kwa upande mmoja, na madereva wa taxi kwa upande mwingine.

Katika kipindi cha miaka 10 hadi kufikia 2018, kulikuwa na ajali 37,421 za bodaboda nchi nzima ambazo zilisababisha vifo 8,000 na majeruhi 35,231 huku baadhi ya majeruhi wakipata ulemavu wa kudumu.

Baadhi ya watumiaji wa usafiri wa Bajaji mjini Moshi wamesema wamekimbia usafiri wa bodaboda kwa kuogopa uendeshaji mbaya.

“Madereva wengi wa bodaboda utadhani wanazaliwa na baba mmoja, mama mmoja,” alisema mkazi wa Shanty Town, Emiliana Johnson.

“Si waangalifu, wana overtake (kupita magari) vibaya kwa kweli mie usafiri wangu sasa ni Bajaji tu.”

Mkazi mwingine wa Moshi anayeishi Pasua, Hamis Abdalah alisema Bajaji hazina rekodi mbaya ya ajali kama bodaboda, na kwamba kadri siku zinavyokwenda usafiri huo unapoteza mvuto.

“Nenda hapo KCMC ukaangalie majeruhi wa ajali. Majority (wengi) kila ukiuliza ni bodaboda. Siwezi kukikimbilia kifo nikikiona. Halafu hata wapewe elimu vipi wanarudi kule kule,” alidai.

Alitaja makosa makubwa ya bodaboda kuwa ni mwendo kasi, kutoheshimu alama za barabarani, kupita magari eneo lisiloruhusiwa, kuchomekea magari na vyombo vyao kutokuwa na bima.

Dereva wa magari ya watalii, Haji Sadick alisema matamko ya kisiasa yamewafanya bodaboda kujiona wako juu ya sheria na wanafanya wanavyotaka kwa vile hivi sasa hawakamatwi tena na trafiki.

“Wewe simama tu hapo barabarani utaona bodaboda wanapita wamepakizana mishikaki au yeye ana abiria wake hawajavaa helmet (kofia ngumu) na hawafanywi kitu,” alidai dereva huyo.

Lakini dereva wa bodaboda kutoka Kata ya Bomambuzi, Charles Mboya, anasema baadhi yao wamesababisha maafa kwa abiria, na hivyo polepole abiria wameanza kuhamia kwenye Bajaji.

“Wewe fuatilia kama utasikia ajali za Bajaji, ni nadra sana kulinganisha na Bodaboda. Ni sisi wenyewe tunavuruga soko letu. Tusipobadilika nakuambia huko mbeleni tutaula wa chuya,” alisema.

Hali inaonekana kuwa mbaya zaidi kwa madereva taxi ambao hulazimika kupiga miayo kutokana na soko lao kuvurugwa na Bajaji ambazo baadhi hupakia abiria katika vituo vya Taxi.

“Tangu Bajaji ziingie taxi utazionea huruma. Dereva Taxi anaweza kukaa kijiweni hata siku tatu hajapakia abiria. Wengi wameamua kuomba kazi gari za utalii,” alisema dereva taxi, Baraka Temba.

“Huu ugonjwa wa Bajaji ni janga la taifa. Arusha hawajaruhusu huu ugonjwa kabisa. Huwezi kukuta Bajaji mjini labda pembezoni mwa mji,” alisema Temba anayeendelea na biashara ya taxi.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini ujio wa Bajaji umekuwa mwiba mkali kwa daladala aina ya Toyota Hiace zinazofanya safari zake KCMC, Kwamtey, Soweto, Rau na maeneo mengine.

Katika maeneo hayo, kumekuwa kukijitokeza migogoro ya mara kwa mara kutokana na kunyang’anyana abiria, ambapo eneo la Pasua, Bajaji bado hazijafanikiwa kujipenyeza.

Wamiliki wa Bajaji wajibu

Chama cha Wamiliki na Waendesha Bajaji na pikipiki cha Kilimanjaro (CWBK) kimewataka madereva taxi na wamiliki wa Hiace kuwa wabunifu wa biashara badala ya kugeuka walalamikaji.

Mwenyekiti wa CWBK, Bahati Nyakiraria alidai Hiace zimepoteza mvuto kwa kukiuka leseni zao kwa kuwaweka abiria vituoni muda mrefu, bila kuzingatia muda na uharaka walionao.

“Hawa Hiace wajue sisi (Bajaji) leseni yetu si ya usafiri wa umma bali ni usafiri wa kukodi. Kwa hiyo mimi hata nikiwa na abiria mmoja tukaelewana bei nakwenda. Wao mpaka wajaze,” alidai.

“Mathalan Hiace inakwenda KCMC inakaa stendi mpaka ijaze abiria wakati kule hospitali kuna muda maalum wa kuona wagonjwa. Hii ndio imewafanya abiria wazikimbe na kuja kwetu,”alisisitiza.

Chanzo: mwananchi.co.tz