Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bajaji 140 zakamatwa Iringa, madereva walalamikia wanaume

Bajaj Pich Bajaji 140 zakamatwa Iringa, madereva walalamikia wanaume

Sat, 4 Mar 2023 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limekamata pikipiki za matairi matatu, maarufu kama Bajaji 140 kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya kupita kwenye njia wasizoruhusiwa, kuzidisha abiria, kuegesha kwenye maeneo waliyozuiwa, kukosa leseni na kupakia mizigo hatarishi.

Kutokana na kamatakamata hiyo iliyofanyika leo Machi 3, 2023 baadhi ya madereva bajaji wa Manispaa ya Iringa wamesema sababu ya kutopita njia waliyotengewa ni uwepo wa matuta mengi yanayolalamikiwa zaidi na abiria wanaume, kwamba yanawaumiza viuno.

Jana Machi 2, 2023 bajaji ziligoma kufanya safari zake kwa madai ya kukamatwa hovyo na kutozwa faini kubwa ya Sh100, 000 huku kupita njia walizo zuiwa ikiwa moja ya makosa.

Hata hivyo, tangu jana jioni baadhi ya bajaji zilitoka mafichoni na kuanza kupakia abiria huku nyingine zikilipisha nauli ya Sh1, 000 badala ya Sh700 ya kawaida.

Wakizungumza, baadhi ya madereva bajaji walijitetea kuwa sababu ya kupita njia walizozuiwa ni uwepo wa matuta mengi.

“Mfano ile njia ya Kihesa inamatuta mengi sana, wanaume wanalalamika kuumizwa viuno vyao ndio maana madereva wengi hatupiti njia hiyo,” alisema dereva bajaji, James Kanyenda.

Kwa upande wa watumiaji wa usafiri huo walisema sakata hilo limesababisha kuchelewa katika shughuli zao za kujiiingizia kipato na wanafunzi kuchelewa ama kutokufika shuleni.

"Tunachelewa katika biashara zetu, watoto wangu ili kufika shule wanategemea bajaji ambazo nyingi zimeshakamatwa" alisema mtumiaji wa usafiri wa bajaji, Idd Nasoro.

Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, Allan Bukumbi amesisitiza kuwa oparesheni hiyo ya kukamata bajaji zinazovunja sheria itaendelea na kuwataka watii sheria bila shuruti.

“Hata hivyo tunaendelea kutoa elimu kwa wamiliki na madereva kuzingatia sheria,” alisema Bukumbi.

Awali, Ofisa Leseni Msaidizi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), Godfrey Calvin wamekuwa wakitoa elimu kwa madereva hao na kwamba, kinachoendelea kwa sasa ni kuwatoza faini wale wanaovunja sheria.

Naye Ofisa Biashara Msaidizi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mkuru Ally alisema kuwa faini ya Sh100, 000 itaendelea kuwepo kwa bajaji zinazovunja sheria.

Chanzo: mwananchi.co.tz