Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bado kuna kero tele za elimu jumuishi wilayani Kilolo

22529 Pic+elimu TanzaniaWeb

Wed, 17 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa muda mrefu kumekuwa na kampeni mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu hasa juu ya haki zao za msingi ikiwamo elimu.

Pamoja na kampeni hizo, bado kilio cha watu wenye ulemavu kupata mahitaji yao muhimu ili waishi kama makundi mengine kwenye jamii hakikomi.

Changamoto lukuki ikiwamo miundombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi wanaoishi na ulemavu, ni moja ya vilio vinavyowafanya baadhi kushindwa kupata elimu.

Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa ni kati ya wilaya zinazokabiliwa na changamoto nyingi katika utoaji wa elimu jumuishi kubwa ikiwa miundombinu isiyo rafiki.

Baadhi ya wazazi wanasema changamoto hizo ndiyo sababu kwa baadhi yao kushindwa kuwapeleka watoto shuleni.

“Nafikiria itakuwaje mwanangu atakapoanza masomo? Mazingira hasa ya vyoo kwenye shule nyingi hasa hapa kijijini hayaruhusu mlemavu kusoma, ni bora nibaki nae nyumbani,” anasema Ivona Kalinga, mzazi wa mtoto mwenye ulemavu anayeishi kijiji cha Nyalumbu wilayani Kilolo.

Anaongeza: “Mwanangu ana miaka minne haoni wala hatembei lakini ana akili vizuri tu kama watoto wengine,” anasema Kalinga.

Kwa mujibu wa jarida ya Shirika la Kuhudumia watoto Duniani (Unicef) , kati ya watoto watano ni wawili tu wapo shuleni.

Sheria namba tisa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010, inataka haki sawa kwa watu wenye ulemavu ikiwamo elimu, ajira, nafasi za uongozi na kuboresha miundombinu.

Hata hivyo, wengi wanakabiliana na miundombinu isiyorafiki ambayo ni kikwazo katika upataji wa elimu.

Jovina Danda, mkazi wa Ilula anasema kama wilaya hiyo isingefanya sensa ya kubaini watoto wenye ulemavu, mwanawe asingempeleka shuleni akihofia miundombinu hiyo isiyo rafiki.

Zamani wanafunzi wenye ulemavu walikuwa wanapelekwa shule maalum lakini kwa sasa, wanasoma elimu jumuishi.

Elimu jumuishi imepewa kipaumbele zaidi kuliko aina nyingine na inachukuliwa kama njia bora zaidi katika kufanikisha malengo ya elimu kwa wote.

Diwani wa kata ya Nyalubu, Dvid Mfungwa anasema miundombinu isiyo rafiki kwenye shule nyingi za msingi na sekondari ni kati ya vikwazo vinavyoikabili elimu hiyo.

Anasema kama suala la miundombinu halitapewa uzito, watoto hao watashindwa kujifunza ipasavyo.

“Ni kweli shule zetu zinakabiliwa na miundombinu isiyo rafiki, hakuna vifaa vya kujifunzia hasa kwa walemavu wasioona, hapa hakuna kujifunza,” anasema na kuongeza;

“Walemavu wa kutoona wanahitaji vifaa maalum ambavyo sio kila shule inavyo, kwa hiyo huyu hatajifunza kama ataingia darasani na kukosa vifaa hivyo.” Anasema.

Mwalimu wa shule ya msingi na ufundi ya Pomerini ambao inatoa elimu jumuishi, Tino Kiponda anasema uhaba wa vitendea kazi kwa wanafunzi wasioona ni changamoto zinazowakabili walemavu hao.

“Ili mtoto mwenye ulemavu wa macho apewe elimu bora, darasa moja wanatakiwa kufundisha walimu wawili kwa wakati mmoja,” anasema.

Anasema uhaba wa walimu ni changamoto nyingine inayoikabili elimu mchanganyiko.

“Kuna watoto wenye ulemavu zaidi ya mmoja kama macho, kusikia na viungo wakati mwingine, huyu hahitaji mwalimu mmoja,” anasema.

Anasema watoto wenye ulemavu wa miguu, wao wanakabiliwa na uhaba wa vibaiskeli, jambo linalowafanya washindwe kujifunza ipasavyo.

Mwalimu mwingine, Justine Kitindasa anasema ili mtoto mwenye ulemavu wa viungo apate elimu bora lazima awe na uhakika wa kutoka hatua moja hadi nyingine kwa baiskeli.

“Kwa hiyo miundombinu kwa watoto wenye ulemavu bado ni shida. Watoto wanahitaji madarasa, walimu wa kutosha, mazingira rafiki ili kupata elimu bora,” anasema Kitindasa

Uongozi wa wilaya wakiri tatizo

Ofisa elimu taaluma Wilayani Kilolo, Biliel Maketa anakiri kuwapo kwa changamoto za kuisukuma elimu hiyo, japo anasema ipo mikakati mingi waliyoiandaa kupambana na elimu hiyo.

Anasema uhaba wa fedha ndio chanzo kikubwa cha changamoto nyingine zote zinazoikabili elimu jumuishi wilayani humo.

“Fedha tunayoipata haitoshelezi mahitaji yote muhimu kwa watoto wenye ulemavu ndio maana kama wilaya tumeanza kubuni njia nyingine za kumaliza changamoto hii,” anasema.

Anasema yapo baadhi ya maeneo hayafikiki kwa gari na hakuna mawasiliano ya simu jambo linalokuwa gumu kufuatilia elimu kwa watoto hao.

Kutokana na changamoto hiyo, Maketa anasema ipo mikakati waliyojiwekea ikiwamo kutoa mafunzo kwa walimu wa kawaida ili wabobee kwenye elimu maalumu.

“Tayari kila kata walimu wawili wameshanolewa na wanafundisha watoto wenye ulemavu,” anaeleza.

Kuhusu miundombinu, Maketa anasema mkakati mkubwa waliojiwekea ni kwa kila mkuu wa shule kuweka kipaumbele kwa watoto wenye ulemavu wakati miundombinu mipya inapojengwa.

Maketa anasema wamekuwa wakifanya vikao na wadau mbalimbali ikiwamo asasi ya Maendeleo ya Watu wa Kilolo (Mawaki) ambayo imesaidia ujenzi wa mabweni mawili kwa ajili ya watoto wenye ulemavu.

Chanzo: mwananchi.co.tz