Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba, mama na watoto wawili wauawa Kasulu Tanzania

90841 Kigoma+pic Baba, mama na watoto wawili wauawa Kasulu Tanzania

Sun, 5 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu wanne wa familia moja akiwamo mme na mke wameuawa na wananchi wenye hasira kali Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma nchini Tanzania wakituhumiwa kujihusisha na imani za kishirikina.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo usiku Jumamosi Januari 4, 2020, Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kigoma, Martin Otieno amesema tukio hilo limetokea Januari 2, 2019 saa 3 usiku.

Kamanda Otieno amesema baba, mama na watoto wawili mmoja wa kike na mmoja wa kiume waliuawa.

“Ni kweli wameuawa wakiwa nyumbani kwao na wananchi wenye hasira kali wakituhumiwa kwa imani za kishirikina ila bado hatujawakamata wahusika,” amesema Otieno

Ametaja majina ya wanafamilia hao ambao ni baba Petro Sagalika anayekadiriwa kuwa na miaka 65-70, mama Suzan Mkuka miaka kati ya 50-55 na watoto Alphonce miaka kati ya 28-30 na Aniza miaka kati ya 38-40.

Otieno ametoa wito kwa wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi na badala yake kuripoti matukio kama hayo pindi yanapotokea katika vyombo husika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

“Tunafanya uchunguzi na upelelezi na tutahakikisha tunawakamata wote waliohusika na tukio hili,” amesema Otieno.

Alipoulizwa kuhusu matukio hayo ya wananchi kuwaua watu wanaohusishwa na imani za kishirikina kwa mwaka 2019, Otieno amesema hana taarifa za matukio hayo.

Chanzo: mwananchi.co.tz