Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba atelekeza watoto 5 alioachiwa

93853 Watoto+pic Baba atelekeza watoto 5 alioachiwa

Fri, 31 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katavi. Sasa ni kama watoto yatima wanaolelewa na mlezi, lakini wazazi wao wako hai.

Watoto hao watano wa familia moja-- wa kwanza akiwa na umri wa miaka 12 na wa mwisho mwaka mmoja, walitelekezwa na wazazi wao kwenye nyumba iliyobomoka iliyo mtaa wa Kazima, Manispaa ya Mpanda mkoani Rukwa na sasa wanalelewa na ofisa mtendaji.

Watoto hao-- Rosemary Lemes (12), Francisco Lemes (8), Selina Lemes (5), Fotunata Lemes (2) na Maria Lemes (1)-- wametekelezwa katika kipindi ambacho tabia hiyo inakua kwa kasi wilayani Mpanda ambako kumeripotiwa zaidi ya matukio 170 kwa mwaka 2019 pekee.

Mtu wa mwisho kuwakimbia watoto hao ni baba yao mzazi, Lemes Kipeta anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (40) ambaye aliondoka zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Hata hivyo, inaaminika kuwa mama wa watoto hao, Faines Francisco alishaondoka muda mrefu baada ya kutengana na mumewe.

Mmoja wa watoto hao, Rosemary aliiambia Mwananchi kuwa mama yao alitengana na baba yao miezi minne iliyopita wakati wakiishi Kawajense baada ya kutofautiana.

Pia Soma

Advertisement
“Siku ambayo mama aliondoka nyumbani aligombana na baba alipokuwa anamuomba hela za kununua chakula, halafu baba akampa Sh20,000, Lakini mama alizikataa kwa sababu alisema ni ndogo hazitoshi,” alisema mtoto huyo.

“Baada ya mama kuzikataa zile hela, baba aliondoka nyumbani na mama naye alipoona baba kaondoka, naye akachukua nguo zake akaweka kwenye mfuko. Tukamuuliza anaenda wapi, akatudanganya anafuata hela kwa baba hakurudi tena.”

Rosemary anasema ilipofika jioni, baba yao alirejea nyumbani na kuwauliza alipo mama yao, wakamjibu hawafahamu.

“Alituchukua akatupeleka kwenye nyumba nyingine tukawa tunakaa huko. Asubuhi akienda kazini alikuwa akirudi usiku huku amelewa chakula chenyewe tulikuwa tunakula mara moja kwa siku na wakati mwingine tunakunywa uji tu. Akawa anatuambia kuna siku nitawaacha peke yenu,” alisema Rosemary.

Baba yao alivyowatelekeza

Mtoto huyo anasema siku ambayo baba yao aliwaacha, alibeba mfuko ambao aliweka nguo zake na walipomuuliza anaenda wapi akawajibu kuwa anaenda kuwatafutia fedha ya chakula.

Rosemary alisema hawajawahi kumuona tena baba yao na msaada mkubwa ulibaki kwa majirani ambao baada ya kubaini kuwa wametelekezwa, wakawa wanawasaidia chakula, siku nyingine walikuwa wakilala njaa.

Mtoto huyo anasema baadaye majirani waliwapeleka ofisi ya serikali ya mtaa kuwaepusha kuendelea kuteseka.

Rosemary, ambaye alitakiwa kuingia darasa la tatu mwaka huu na Francisco darasa la pili katika Shule ya Msingi Makongoro, wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na baba yao kushindwa kuwatimizia mahitaji ya shule na tabia ya kuhama makazi mara kwa mara.

Majirani wasimulia

Majirani wa familia hiyo, Happyness Alphonce na mumewe Filberth Mangasini, waliliambia Mwananchi kuwa baba wa watoto hao alikuwa na wake wawili baada ya kuachana na mke mkubwa, aliwachukua watoto na kuwapeleka kwa mke mdogo.

“Mke mdogo ilibainika alikuwa mke wa mtu, baadaye naye aliondoka, baba huyo akaendelea kuishi na watoto wake kwenye nyumba hiyo, ikafikia hatua akaomba akabidhi watoto kwetu tukakataa.

“Siku chache baadae akawa haonekani, watoto wakawa wanashinda na njaa wakaanza kuokota chakula jalalani,” alisema.

“Tukapata hofu wanaweza kufanyiwa vitendo vya kikatili au kuangukiwa na ukuta wa nyumba hiyo, tukaomba barua kwa mjumbe na kuwapeleka kwa Mwenyekiti wa mtaa,” alisimulia Mangasini.

Serikali ya mtaa

Mwananchi ilizungumza na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kazima, Flaviana Salala anayeishi na watoto hao kwa sasa, alisimulia alipokea taarifa hizo kutoka kwa majirani wa familia hiyo kuwa wametelekezwa na wanaishi kwenye mazingira hatarishi kulingana na umri wao kuwa mdogo.

“Nimewapokea kutoka kwa majirani wakiwa na barua ya mjumbe, sasa kama mzazi ninawasaidia, ninachokula na wao wanakula, nimeripoti polisi wakashauri niwapeleke ustawi wa jamii, najiandaa kufanya hivyo, lakini kitendo hiki hakifai niwashauri wazazi ukizaa uwe tayari kulea,” alisema Flaviana.

Naye mkuu wa wilaya, Lilian Matinga alisema hana taarifa hiyo na kuahidi kufuatilia suala hilo ili ikiwezekana watoto hao wapelekwe kwenye kituo cha kulelea watoto yatima na wale wanaosoma watatafutiwa shule.

“Mwandishi nimepokea taarifa hizi kutoka kwako kwa masikitiko makubwa nitafuatilia kwa kushirikiana na ofisi ya ustawi wa jamii ili wapelekwe sehemu husika na wazazi watatafutwa hadi wakamatwe na vyombo vya dola, nitoe wito wazazi tusikwepe majukumu, viongozi wa dini watusaidie kukemea tabia hii makanisani ili ikome maana imekithiri,” alisema Matinga.

Ofisa Ustawi wa jamii wa mkoa wa Katavi, Bahati Mwailafu alipozungumza na Mwananchi alisema mkoa huo umekuwa na matukio mengi ya kutelekeza watoto.

Alitoa mfano kuwa mwaka 2019, matukio ya wazazi kutelekeza watoto yaliyoripotiwa yalikuwa 179.

“Hii tabia ipo na inasababishwa na uelewa mdogo wa wazazi/walezi kutofahamu wajibu wao na haki za mtoto, matukio yanayoripotiwa ni machache na mengi hayaripotiwi,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz