Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba asimulia ulezi ulivyo na changamoto

68449 Baba+pic

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukimuangalia kwa haraka mtoto Asha (siyo jina halisi) unaweza kufikiri ana umri wa miezi sita kwa muonekano wake badala ya mwaka mmoja.

Asha amepatwa na hali hiyo kutokana na kwamba, alikuwa hatarini kupata udumavu baada ya uzito wake kushuka.

Mtoto huyo ambaye jina lake tumehifadhi kwa mujibu wa sheria, alifiwa na mama yake akiwa na siku nne tangu azaliwe na kulelewa na baba yake ambaye uzoefu kuhusu lishe ya mtoto ulikuwa mdogo.

Kutokana na hali hiyo, Asha ilimlazimu kupata maziwa ya ng’ombe mara tatu kwa siku badala ya mara 12 na wakati huohuo maziwa hayakutengenezwa kwa hali ya usafi na mchanganyiko wa maji kama ilivyotakiwa.

Kitaalamu ili mtoto asipate udamavu, mzazi na watoa huduma hutakiwa kuzingatia lishe bora kwa siku 1,000 tangu kutungwa kwa mimba.

Baba wa mtoto huyo, Hussein Saidi mkazi wa Singida, anasema baada ya kufiwa na mke wake, aliachiwa watoto wawili ingawa bibi wa watoto hao angepaswa kutoa msaada kwenye malezi ya watoto, lakini ni mlemavu wa macho.

Pia Soma

Kutokana na hali hiyo, Saidi alijikuta katika kitendawili baada ya kushindwa kufuata taratibu za lishe na kusababisha uzito wa mtoto kushuka.

Anasema baada ya mke wake kufariki dunia alilazimika kushika nafasi mbili yaani baba na mama kwa mtoto wake Asha.

“Nilijitahidi kununua maziwa ya ng’ombe, lakini mtoto alianza kuharisha na baada ya kupata utaalamu wa daktari nilibaini kuwa nilikuwa sichanganyi maziwa na maji ipasavyo.

“Maisha yamekuwa magumu mno, mimi ni mkulima natakiwa nilime ili nipate kipato cha kuhudumia familia yangu, lakini wakati huohuo natakiwa kuwalea watoto wangu pamoja na mama yangu kipofu, jambo ambalo limekuwa gumu kidogo na uzito wa mtoto wangu ukashuka sana,” anasema.

Wataalamu wanasemaje?

Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Ilongero, Grace Kishindo anasema Saidi alimpeleka kituoni mtoto wake akiwa na miezi sita, anaumwa na uzito wake ukiwa umeshuka.

Anasema walianza kumfuatilia kwa karibu mtoto na kumwelimisha baba namna ya kumlea mtoto ikiwa ni pamoja na kuzingatia usafi wa vyakula na jinsi ya kuchanganya maziwa ya ng’ombe na maji kwa kuwa yana protini nyingi kuliko ya mama.

Dk Kishindo anasema kwa sasa mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja ana uzito wa kilo 7.5 ambao ni pungufu ya kilo tano kwa kuwa mtoto wa mwaka mmoja anapaswa kuwa na angalau kilo 12.

“Siku 1,000 za mtoto tangu kutungwa mimba ni muhimu sana kwa ukuaji bora wa mtoto (kuzingatia lishe) na makosa yakifanyika kuna hatari ya kupata utapiamlo au udamvu, hata hivyo tunaimani kwa kuwa tumeanza kumtibu mtoto mapema tunaweza kufanikiwa kumuokoa na udumavu,” anasema Saidi.

Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa za Utafiti wa Hali ya Afya (TDHS), Tanzania ina kiwango cha juu cha utapiamlo mkali.

Asilimia 34 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wamedumaa.

Lishe duni nayo ni tatizo miongoni mwa wanawake walio katika umri wa kuzaa.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Singida ni miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya watoto wenye utapiamlo hasa wa udumavu.

Katika mkoa huo udumavu upo kwa asilimia 29.2 na utapiamlo asilimia 4.7, ikilinganishwa na takwimu za kitaifa ambazo udumavu ni asilimia 34 wakati utapiamlo ni asilimia 4.4.

Kutokana na changamoto hiyo, hivi sasa kuna mradi wa Boresha Lishe wa miaka mitano kuanzia mwaka 2016 hadi 2021.

Mradi huu unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya(EU), una lengo la kuimarisha lishe na kuboresha uhakika wa chakula.

Kwa Tanzania, mradi umejikita kuzuia udumavu, kutibu utapiamlo, kuimarisha ukusanyaji na matumizi ya takwimu za lishe na kukuza uelewa wa maarifa ya lishe kwa jamii za wenyeji na watumishi wa ngazi za mkoa na wilaya katika maeneo ya mradi.

Pia, umelenga kubadilisha tabia za kijamii zinazozuia lishe njema, uzalishaji na usambazaji wa vyakula mchanganiko na vyenye virutubisho maalumu katika wilaya za Bahi na Chamwino mkoani Dodoma pamoja na wilaya za Ikungi na Singida Vijijini mkoani Singida. Kati ya bajeti ya Euro 24.5millioni; EU imetoa Euro 9.5milioni lakini bado kuna upungufu wa Euro 15.0 milion.

Ofisa Lishe wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani ( WFP), Neema Shosho anasema kupitia mradi wa Boresha Lishe wamefanikiwa kusambaza vyakula maalumu vilivyoongezwa virutubisho kwa ajili ya wajawazito, wanaonyonyesha pamoja na watoto wenye umri chini ya miaka miwili.

Humphrey Chilewa kutoka Taasisi ya Research Community and Organization Development Associates (Recoda) mkoa wa Singida, anasema wanatekeleza kipengele cha kilimo na ufugaji ili kuwa na uhakika wa chakula na lishe katika ngazi ya kaya.

Anasema wameongeza kilimo cha mbogamboga na mazao mengine ili kuhakikisha uhakika wa chakula.

“Tulianza kutoa elimu Oktoba 2017 na tunatoa elimu za kilimo bora kwa ujumla wake kuhakikisha kila kaya inakuwa na uhakika wa chakula,” anasema.

Mratibu wa lishe Wilaya ya Ikungi, Mkoa wa Singida, Agnes John anasema mradi wa Boresha Lishe ulioanzishwa na WFP unalenga kuhakikisha upatikanji wa lishe na virutubisho katika ngazi ya kaya.

Anasema mradi huo umewalenga mama na mtoto na umegawanyika katika maeneo mawili pamoja na ngazi ya jamii na huduma.

Akifafanua anasema kwa mwaka wa 2018/19 halmashauri kupitia vyanzo vyake vya ndani imeweza kutenga milioni 57 kusaidia katika masuala ya lishe.

Elimu wa wananchi kuhusu lishe

John anasema wanatoa elimu ya kuwa na bustani ya mboga mboga kwa kutumia maji machache kwa kuwa mkoa wa Singida huwa una changamoto ya ukame kwa takribani miezi mitano kila mwaka.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Singida Rashid Mandoa amesema mkoa wa Singida hutumia kilimo cha samadi.

Anasema mkoa huwa una changamoto ya kuwa na utapiamlo ukiokithiri licha ya kuwa upatikanaji wa chakula mchanganyiko wakiwamo kuku wa asili, mboga mboga tofauti na matunda.

Rashid anasema kuanzisha elimu kwa lengo la kuwapa uwezo wakazi wa aneo hilo kuelewa vyakula ni muhimu kwa lishe bora kwa watoto na watu wazima.

Chanzo: mwananchi.co.tz