Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba akimbia mke, mtoto mwenye uvimbe tumboni

Mtoto Uvimbe Tumboni Baba akimbia mke, mtoto mwenye uvimbe tumboni

Sun, 9 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkazi wa Kitongoji cha Msufini kilichopo katika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Leokadia Said (28) amewaangukia Watanzania na Serikali akiomba msaada wa matibabu ya mwanaye mwenye uvimbe kwenye kitovu.

Uvimbe huo umesababisha ukuaji wa mtoto huyo, Mastidia Derick, mwenye umri wa miezi sita kuzorota na hivyo kuhitaji matibabu ili kurejesha afya yake na ukuaji wenye siha kama watoto wengine wanaozaliwa hapa nchini.

Licha ya kulazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Francis tangu alipojifungua mtoto huyo, mume wake ambaye wamezaa naye watoto wawili alimtelekeza na kujikuta akidaiwa deni kubwa katika hospitali hiyo.

“Kwa muda niliokuwa nimelazwa hospitali ya Mtakatifu Francis, mume wangu ambaye tumezaa watoto wawili, hakuwahi kuja hata kunitembelea, badala yake aliamua kunikimbia na kuondoka, nasikia yuko Iringa,” amesema Leokadia.

Amesema deni liliongezeka hadi kufikia Sh780,000 lakini yeye na familia yake walilipia na kubalia Sh285,000. Kwa kuwa hakuwa na fedha, aliambiwa na viongozi wa hospitali kwamba arudi nyumbani, atakuwa akienda hospitali hapo kwa ajili ya vipimo kila baada ya siku 14.

Mwanamke huyo amebainisha kwamba kwa sasa hali yake ya kiuchumi ni mbaya, hakupata hata nauli ya kurudi tena hospitali tangu wakati huo ikiwa imepita miezi mitatu na uvimbe unaongezeka kuwa mkubwa tofauti na awali.

“Mwanangu huyu anasumbuliwa na changamoto ya uvimbe ulitokea kwenye kitovu baada ya kuzaliwa, kila kukicha uvimbe unaongezeka na kila kukicha natumia Sh3,000 kumpeleka duka la madawa ili akafungwe kitambaa maalumu eneo hilo la uvimbe ili lisiingiliwe na uchafu. Uvimbe unazidi kuwa mkubwa, naomba msaada mwanangu atibiwe,” amesema.

Amesema wakati mtoto anazaliwa, alifanyiwa upasuaji kutokana na kutokana na changamoto yake ya kiafya, walitenganishwa wodi ambapo alikaa mwezi mmoja na siku 14 bila kumnyonyesha mtoto wake huyo, jambo ambalo sio la kawaida.

Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, kata ya Sanje, Godfrey Sambu ndiye aliyeibua changamoto ya mtoto huyo baada ya kumtembelea mama huyo na kumshauri kutafuta msaada kwa ajili ya matibabu ya mtoto wake.

“Nikiwa natekelea majukumu yangu kwenye mikutano mbalimbali nilipokea taarifa kutoka kwa raia mwema akiniambia kuna mama kwenye kata yetu ana mtoto mgonjwa na mara nyingi huwa anawekwa ndani na hatoki nje. Kwa haraka nilifika kwenye hiyo nyumba, nikamuona yule mama mwenye mtoto na kuongea naye, baada ya kusema naye kwa muda akamtoa mtoto wake, nilipomuona ndipo nikatoa taarifa ili aweze kupata msaada,” amesema.

Kwa sasa Leokadia hafanyi shughuli yoyote ya kumuingizia kipato badala yake anakaa nyumbani na mtoto wake muda wote, jambo linalomfanya awe tegemezi kwa mama yake mzazi.

“Kwa sasa siwezi kufanya kazi yoyote kutokana na hali ya mwanangu ilivyo, nalazimika kukaa na mtoto wangu muda wote na hata fedha za kumfunga kitamba huwa ananipa mama yangu mzazi (65) ambaye analima vibarua kwa ajili ya kunisaidia. Kutokana na hali hii, naomba msaada Watanzania wanisaidie mwanangu apate matibabu,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msolwa Ujamaa, Alex Kingonda amesema alipata taarifa kuwa Leokadia amekimbiwa na mumewe akiwa na mtoto mgonjwa.

“Tulipata taarifa za ugonjwa wa huyu mtoto kutoka kwa mama yake, lakini akalalamika kuwa amekimbiwa na mumewe, tuliwasiliana nae akaahidi kurudi kulea familia lakini hajarudi hadi leo, hivyo tumeshaanza utaratibu wa kumkamata kwa ushirikiano na jeshi la polisi ili arejee kusaidia malezi ya huyu mtoto wake ambaye ni mgonjwa.

“Ninawaomba wananchi wengine wenye watoto wenye changamoto kwenye maeneo yao wawaibue mapema ili waweze kupatiwa matibabu kwani ukikaa na mtoto mgonjwa kwa muda mrefu bila kupata matibabu unazidisha ugonjwa,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live