Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baada ya dhiki, kivuko kipya Ukara kuinua uchumi

B3d7309998756db21ecbb04bd52a5b47.png Baada ya dhiki, kivuko kipya Ukara kuinua uchumi

Tue, 3 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NI miaka miwili na nusu sasa tangu wananchi wa Ukara, wilayani Ukerewe mkoani Mwanza walipokumbwa na janga la kupoteza ndugu, jamaa na marafi ki baada ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere, Septemba 20 mwaka 2018.

Katika tukio hilo baya watu takribani 227 walipoteza maisha. Taarifa zilizotolewa na Serikali juu ya sababu za kuzama kwa kivuko hicho kilichokuwa kinatoa huduma ya usafiri kati ya kisiwa cha Bugorola na Ukara ni pamoja na kubeba wasafiri wengi na mizigo kinyume na uwezo wake.

Mv Nyerere ilikuwa na uwezo wa kubeba tani 25, abiria 101 na magari madogo manne pekee lakini siku hiyo idadi tu ya waliokufa ni zaidi ya watu 200.

Hata hivyo, wananchi wa Ukara na wale wa maeneo jirani, sasa watapata ahueni baada ya Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kununua kivuko kipya cha Mv Ukara-II, (Hapa Kazi Tu) kilichozinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe anasema baada ya kutokea kwa ajali hiyo, Rais John Magufuli ambaye amechaguliwa tena na Watanzania kwa kishindo kuendelea kuongoza nchi, aliiagiza wizara yake kununua na kupeleka kivuko kingine ili shughuli za uzalishaji mali za wananchi kwenye kisiwa hicho ziendelee.

Wakati kivuko kipya kikitayarishwa, kivuko cha Mv Sabasaba chenye uwezo wa kubeba tani 85 (abiria 330 na magari madogo sita), boti ya Mv Ukara yenye uwezo wa kubeba abiria 25 pamoja na boti ya utafiti na uokoaji SAR-3 zilipelekwa kisiwani humo kutoa huduma ya usafirishaji.

Waziri Kamwelwe anamshukuru Rais Magufuli kwa uongozi wake mahiri, wa kizalendo na wenye upendo mkubwa, unaomsukuma kujenga na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo iliyopo hapa nchini ikiwemo ya ununuzi wa kivuko hicho.

“Ninafarijika kuona kuwa ndani ya kipindi kisichozidi miaka miwili, tumetekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais na sasa kivuko kimeanza kufanya kazi,” anasema.

Anasema kivuko hicho kipya ni cha kisasa zaidi, kimehakikiwa ubora wake kiusalama na kimewekewa vifaa maalumu vya kujiokolea wakati wa dharura.

Kina urefu wa mita 42 na upana wa mita 10 na kimesanifiwa kubeba tani 100, yaani abiria 300 na magari madogo 10.

“Kivuko hiki kimeongezewa uwezo wa kubeba mizigo tofauti na kile cha zamani cha Mv Nyerere kilichopata ajali ambacho kilikuwa na uwezo wa kubeba tani 25 tu za mizigo, abiria 101 na magari madogo manne na ununuzi wake umegharimu Sh bilioni 4.2, fedha za walipa kodi kwa asilimia 100,” anasema.

Anasema ujenzi wa kivuko hicho umefanywa na mkandarasi mzawa, Kampuni ya Songoro Marine Transport Limited ya jijini Mwanza kwa kutumia rasilimali za ndani za nchi ni jambo la kujivunia kwa nchi kutumia rasilimali hizo kuboresha maisha ya watanzania kiuchumi na kijamii kwa kuweka miundombinu wezeshi ikiwemo hiyo ya vivuko.

“Hili ni jambo jema tunalotakiwa kuliendeleza kwa kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wao kwa kuhakikisha wanashiriki katika shughuli za ujenzi ikiwemo utengenezaji wa vivuko,” anasema.

Anasema kuwa ni imani yake na ya Wizara, kupitia mradi huo kuwa wapo watanzania wengi waliopata fursa ya kujenga na kuunganisha kivuko hicho na kwamba wamejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na teknolojia ya ujenzi wa vivuko.

“Ninaamini kuwa ujuzi, uzoefu na kipato walichokipata kitaboresha hali ya maisha yao na wataendelea kutoa mchango kwa taifa,” anasema na kuwapongeza watendaji wa wizara yake kwa kuendeleza utaratibu huo wa kujenga vivuko kwa kutumia mkandarasi wa ndani, hatua ambayo imewezesha kupata huduma nzuri ya usafiri, kuongeza teknolojia na ajira kwa vijana.

Anasema kuanza kutumika kwa kivuko hicho, ambacho ni kati ya vivuko vinne vipya vilivyonunuliwa na serikali katika ziwa Victoria, kuna manufaa makubwa sana ya kiuchumi kwa wananchi wa Ukara na Bugorola ikizingatiwa kuwa kivuko kilichokuwepo kilipata ajali.

“Kivuko hiki kipya kitawasaidia wananchi kusafiri na kufanya biashara katika maeneo ya visiwa vya Ukerewe na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, usafirishaji wa bidhaa na vyakula kama sehemu ya mahitaji muhimu kwa jamii,” anasema.

Waziri Kamwelwe ametoa maagizo kwa Wakala wa Meli Nchini (TASAC) kuhakikisha inaweka maofisa usimamizi katika maeneo yote ya usafiri wa majini, na kutoa mafunzo kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya majini akiwemo Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).

Anasema hatua hiyo itasaidia kuongeza ufahamu juu ya umuhimu wa kuzingatia utaratibu na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa vyombo hivyo ili kuepuka matukio ya ajali.

Aidha, ameiagiza TEMESA kusimamia kwa ukaribu uendeshaji wa vivuko hivyo ili wananchi wafaidi matunda mazuri ya serikali yao kwa fursa ya maendeleo yao binafsi na kuwahakikishia wakazi wa Ukara kuwa kivuko hicho kina ubora kwa kuwa kimewekewa mfumo maalumu ambao unaweza kutambua uzito.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia (Sekta ya Ujenzi), Elias Mwakalinga anasema katika kuhakikisha usafiri wa vivuko unakuwa ni wa uhakika muda wote na salama, Serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni 1.44 katika mwaka wa fedha 2020/21 kwa ajili ya uwekaji wa mfumo wa kielektroniki kwenye vivuko vyote nchini kwa ajili kudhibiti ajali kwenye vivuko na idadi ya abiria na mizigo itakayokuwa ikisafirishwa kupitia kwenye vivuko hivyo.

Mwakalinga anasema kupitia mfumo huo, ambao utaunganishwa kwenye ofisi za Wizara ya Ujenzi, utawekwa katika ofisi ya Waziri mwenye dhamana ofisini kwake na watendaji wa juu wa Wizara na kwamba vivuko na meli zitakazokuwa zikisafiri bila kuzingatia idadi ya abiria na mizigo inayotakiwa safari zitasitishwa mara moja na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha inaondoa kabisa changamoto ya usafiri wa majini, kupitia mfumo huu hata kama wananchi wataingia kivukoni wakiwa wamezidi, mfumo huu utagundua na sisi tutapata taarifa,” anasema.

Sambamba na hatua hiyo, Mwakalinga anasema Serikali imekamilisha ujenzi wa vivuko saba vyenye thamani ya Sh bilioni 36.4 ukiwemo ujenzi wa ambulance maalumu tatu kwa ajili ya kusaidia usafiri wa majini katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella anaamini kivuko hicho, kitaboresha biashara na kuimarisha vipato vya wananachi kwa kuwa usafiri ni sekta nyeti kwa maendeleo.

Anawataka wananchi hao kukitumia kivuko hicho vizuri katika uzalishaji ili kupandisha uchumi wao. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, ambaye mkoa wake utanufaika pia kiuchumi na ujenzi wa vivuko hivyo, anasema kuzinduliwa kwa kivuko hicho ni nuru kwa wakazi wa maeneo ya Ukerewe na wilaya jirani za mkoa wake.

Malima anasisitiza kuwa watanzania ni wamoja na hivyo wasiyakubali maneno ya kutenganishwa yanayotolewa na baadhi ya watu bali waimarishe umoja na mshikamao.

Mkuu wa wilaya ya Ukerewe, Cornel Maghembe anasema tangu ilipotokea ajali ya Mv. Nyerere mwaka 2018 wananchi walikabiliwa na shida ya usafiri na kwamba wanaishukuru serikali ya awamu ya tano inayosema na kutenda.

“Kwa niaba ya wananchi, wanatoa shukurani kwa Rais John Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa ili kitatatua changamoto ya usafiri katika eneo hili.

Sasa wamepata kivuko kitakachotumia dakika 40 tu kutoka Bwisya kwenda Bugolola ambapo awali walitumia saa mbili,” anasema Maghembe.

Mtendaji Mkuu wa Temsa, Japhet Maselle anasema kivuko hicho kimejengwa kwa umbo la meli ili kuzingatia mahitaji ya aina ya huduma inayotolewa kwa sasa na baadaye katika usafirishaji wa mizigo, abiria na magari.

“Kivuko hiki kimefungwa injini mbili aina ya Dosan Infracose zenye uwezo wa horse power 360 kila moja na kinaendeshwa na mifumo mitatu ya usukani,” anasema na kuongeza kuwa kabla hakijaanza kazi kilifanyiwa ukaguzi wa mwisho na Shirika la Uwakala wa Meli nchini (TASAC) ambapo ubora wa viwango vya usalama wa abiria, magari na mizigo ulithibitika.

Baadhi ya wakazi wa Ukara na Bugorola wilayani Ukerewe wanamshukuru Rais Dk John Magufuli kwa ujenzi wa kivuko hicho ambacho wamekifananisha na ujio wa ndege mpya iliyonunuliwa na Serikali kisiwani humo kutokana na ubora wake.

Chanzo: habarileo.co.tz