Ilikuwa Mei 18 mwaka huu siku ambayo ilizuka taharuki na sintofahamu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro baada ya mwili wa mzee Melkiori Ndambale (85) uliokuwa umehifadhiwa katika hospitali hiyo kutoonekana kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.
Siku hiyo ndugu wa marehemu huyo mzee walifika katika chumba hicho cha kuhifadhia maiti kwa lengo la kuchukua mwili kwa ajili ya maziko na kuukosa mwili wa mpendwa wao, jambo lililosababisha uongozi wa hospitali kuusaka.
Maulid Ndambale ni mdogo wa marehemu amesema kuwa baada ya uongozi wa hospitali kufuatilia katika vitabu kumbukumbu, ilifahamika kuwa mwili wa kaka yake ulichukuliwa na familia moja ambayo nayo ilikuwa na imemuhifadhi baba yao katika chumba hicho na kisha kwenda nao wilayani Kilosa kwa ajili ya maziko.
"Tukiwa pale pale mochwari tukapata taarifa kuwa tayari baba yetu huko Kilosa na kwamba tayari alikuwa keshazikwa tena kwa dini ya kiislamu, na ilionekana kuwa hao watu wa Kilosa waliuacha mwili wa baba yao hapa hapa mochwari," amesema Ndambale.