Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aweso awapa Dawasa siku tatu kuhakikisha maji yanafika Kisarawe

Aweso awapa Dawasa siku tatu kuhakikisha maji yanafika Kisarawe

Thu, 31 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kisarawe. Naibu Waziri wa Maji nchini Tanzania, Juma Aweso ametoa siku tatu kwa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) kuwasha mtambo wa maji ili wananchi wa Wilaya ya Kisarawe wapate maji.

Mtambo huo ulitakiwa kuwashwa leo Jumatano Oktoba 30, 2019 lakini imeshindikana kutokana na mtambo wa Kibamba kutofungiwa umeme ili mashine ziweze kusukuma maji mpaka Kisarawe.

Aweso amewahoji watendaji mbalimbali kuhusu kukwama kwa mradi huo ulioanza mwaka 2014 ambao umekamilika kwa asilimia 99 huku tatizo likitajwa kuwa ni umeme.

"Haiwezekani tuendelee kupiga danadana tu wananchi wanataka kuona maji na si sababu mnazozitoa. Nataka kuona wananchi wanaanza kupata maji ndani ya siku tatu, kuunganisha umeme ni jambo dogo sana," amesema Aweso.

Naibu waziri huyo ameahidi kufikisha maji katika shule ya sekondari ya Pugu na sekondari ya Chanzige kupitia mradi wa maji wa Kisarawe – Pugu.

"Kupitia mradi huu nimewaagiza Dawasa walete maji hapa (shule ya Pugu). Mimi nimesoma hapa najua shida ya maji, wakati fulani ilikuwa kuoga mpaka uteremke nyumbani huko mitaani,” amesema Aweso. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo akizungumzia changamoto ya maji wilayani humo amesema walikuwa nyuma kwa sababu hakukuwa na maji safi na salama.

Amebainisha kuwa tanki la maji lililojengwa kwa Sh10.6 bilioni litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 6 za maji kwa siku, wakati mahitaji ya maji katika wilaya hiyo kwa siku ni lita milioni 1.2.

“Tunatarajia maendeleo yatakua kwa kasi kwa sababu tutakuwa na maji ya kutosha, wawekezaji watakuja wa kutosha. Nimeagiza halmashauri ya wilaya ya Kisarawe kuanza kupima viwanja, hatutaki mambo ya squatters tena," amesema Jokate.

Kaimu mkurugenzi wa miradi ya Dawasa, Ramadhan Mtindasi amesema mradi huo umekamilika kwa asilimia 99 na mpaka sasa wamelaza bomba la kilomita 34.

Amebainisha kuwa ndani ya siku tatu watakuwa wamekamilisha mradi huo na katika awamu ya kwanza watawaunganisha wananchi 1,000 kwa mkopo na watatakiwa kulipa kidogo ndani ya miezi 12.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz