Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Avunjwa mguu, mkono na tembo

D996E2BD C40C 4E12 8CF8 8B6C9750785B.jpeg Tembo ajeruhi Handeni

Sun, 28 Aug 2022 Chanzo: Mwananchi

Mkazi mmoja wa kijiji cha Kiseriani kata ya Kwamatuku wilayani Handeni mkoani Tanga, Samwel Losambo amejeruhiwa na tembo kwa kuvunjwa mguu na mkono baada ya tembo kuvamia kwenye mashamba katika kijiji hicho.

Akizungumza leo Jumapili Agosti 28, 2022 diwani kata ya Kwamatuku, Mustaph Beleko amesema mwananchi huyo alijeruhiwa wakati akijaribu kuwaswaga tembo hao kutoka ndani ya kichaka.

"Majeruhi amevunjwa mkono wa kushoto, amepasuliwa mguu wa kushoto na eneo la kifuani upande wa kulia pia kajeruhiwa, tembo hawa wanakuja mpaka ofisini kwangu na baadaye wanarudi tena kwenye msitu wa eneo hilo", amesema Beleko.

Amesema hali ni tete hapo Kwamatuku na hivyo kuomba wananchi wasaidiwe kwani uwepo wa tembo hao kwenye makazi yao utaweza kuleta madhara zaidi kwa wananchi wake na mazao.

Beleko ameongeza kuwa amewasiliana na TAWA ila majibu yao sio ya kuridhisha kwamba wataweza kusaidia wakati hawana mafuta kwaajili ya shughuli hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe amesema hatua za haraka zitachukuliwa na mamlaka husika huku akisema kuwa TAWA hawampi ushirikiano wa kutosha kwenye tatizo hilo.

"Labda nimuombe mkuu wa mkoa aingilie kati kuhusu wenzetu wa TAWA maana kila ukiwasiliana nao wanasema tunakuja ila hawafiki, wananchi wangu wanaishi kwa mashaka kwenye maeneo yao huku mazao yakiharibika hili sio sawa wanatakiwa kuwajibika", amesema DC Mchembe.

Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Handeni, Ali Mkobe ambaye anaishi eneo hilo amesema wameshamsafirisha majeruhi huyo kwenda hospitali ya Magunga Korogwe kwaajili ya matibabu.

Jana Tembo wengine walionekana katika kijiji cha Nkale kata ya Segera ambapo walishambulia michungwa na mikorosho.

Chanzo: Mwananchi