Serengeti. Mkazi wa kijiji cha Bukore kata ya Kyambahi wilaya ya Serengeti, Motondi Shakanyi (26) ameuawa na tembo wakati wakisaidiana na ndugu zake kuwafukuza wanyama pori hao shambani.
Mkuu wa wilaya hiyo, Nurdin Babu ameithibitishia Mwananchi kutokea kwa tukio hilo leo Mei 27, 2019 wakati wakifukuza tembo kwa kupiga madebe.
Babu amewaomba wananchi kutoa taarifa kwa viongozi ili askari wawe wanafika kuwasaidia kuwaondoa ili kuepusha madhara kama hayo yanayoweza kutokea.
Karela Nzumbe kaka wa marehemu amesema baada ya tembo kuingia yeye na mdogo wake wa kiume walitoka na kumwambia mama yao abaki na huyo marehemu ambaye ni mwanamke.
"Kwa kuwa ilikuwa giza na hatuna tochi na eneo la shamba liko mbali na nyumbani mama na dada tuliwakataza kutoka, lakini nao waliamua kuja ndipo akakutana na tembo akamshika na kumrusha kama hatua 50 na kufa papo hapo," amesema.
Amesema wakati tukio linatokea wao walikuwa wakihangaika kutoa kundi la tembo zaidi ya 10 kwenye shamba moja na walipotaarifiwa kufuatilia wakakuta ameshakufa.