Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Auawa kwa risasi akikata kuni shambani

RISASI 2222222222 Auawa kwa risasi akikata kuni shambani

Mon, 14 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mtu mmoja wilayani Muheza mkoani Tanga amefariki dunia baada ya kudaiwa kupigwa risasi kifuani na mlinzi wa shamba la Magoroto Estate wilayani Muheza, Samson Steven wakati akiokota kuni kwenye shamba hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Henry Mwaibambe alithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema kuwa kufuatia tukio hilo, wanamshikilia Samson Steven ambaye ni mlinzi wa shamba hilo kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

Kamanda Mwaibambe alimtaja marehemu aliyepigwa risasi wakati akiokota kuni ni Athumani Ramadhani ambaye baada ya kupigwa risasi ya kifuani alifariki dunia papo hapo.

"Kwa kweli hili ni tukio la kusikitisha na hivi sasa Jeshi la Polisi tunamshikilia mtuhumiwa ili kujibu tuhuma zinazomkabili za kufanya mauaji kwa raia," alisema Kamanda Mwaibambe.

Kiongozi huyo alisema kuwa maelezo ya mtuhumiwa ni kwamba alimpiga risasi ikiwa ni sehemu ya kujihami baada ya kumkamata kwa kuingia kwenye shamba hilo kinyume cha taratibu.

Alisema mtuhumiwa huyo katika maelezo yake kwa polisi, alidai wakati akijaribu kumtia nguvuni, alitaka kumvamia na ndiye alifyetua risasi.

Kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa iwapo kunatokea vitendo vya uhalifu, wanapaswa waripoti kwenye mamlaka husika ili zichukue hatua.

Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania toleo la mwaka 1977, inaeleza: "Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria".

Chanzo: www.tanzaniaweb.live