Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Auawa kwa kuchomwa moto tuhuma za wizi

ACP Pili Mande Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP Pili Mande.

Fri, 21 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi waliotajwa wenye hasira kali Manispaa ya Lindi mkoani hapa, wamemuua kwa kumchoma moto kijana ambaye jina na mahali anakoishi hakujafahamika, baada ya kudaiwa kuiba vyombo vyenye thamani ya Sh. 85,000 nyumbani kwa Pili Ally.

Tukio la kuuawa kijana huyo mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya 30 na 32 limethibitishwa na mamlaka husika. Lilitokea Julai 14, mwaka huu katika Mtaa wa Mangomboli mjini Lindi.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamedai kuwa siku hiyo, mtuhumiwa kabla ya kukutwa na umauti, aliingia ndani ya nyumba ya mama huyo kisha kuiba fedha na vyombo vya kupakulia vyakula (ho pots) wakati mmiliki huyo akiwa amekwenda bombani kuteka maji.

Walidai kuwa wakati kijana huyo akiwa anatoka ndani ya nyumba hiyo, alikutana na mama mlangoni kisha kumsukuma na kudondoka chini na kukimbilia nje, jambo ambalo lilimfanya Pili apige kelele kuomba msaada wa wananchi wenzake walijitokeza na kumshushia kipigo kijana huyo.

“Huyu mama wakati anarejea alimkuta mwizi anatoka ndani mkononi akiwa ameshikilia poti akitoka nje na kusukumwa na kudondoka chini, akapiga kelele za mwizi,” walidai Daudi Mbuyu na Happy John, wakazi wa eneo hilo.

Pili ambaye ni mmiliki wa nyumba hiyo, akizungumza kabla ya askari kuwasili eneo la tukio, alidai kijana huyo alimkuta ameibia fedha taslimu Sh. 85,000, vyombo vitatu vya kuwekea chakula na redio moja.

Alisema ni mara ya pili kwake kumkuta kijana huyo akiwa ndani ya nyumba yake akiwa anamwibia, lakini alikuwa anazidiwa nguvu na kibaka huyo kwa kumsukuma na kudondoka chini na kutoa nafasi ya kutokea nje na kukimbia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP Pili Mande, alithibitisha kutokea mauaji ya kijana huyo asiyefahamika jina wala mahali anakoishi na kueleza mwili wa mtuhumiwa huyo umepelekwa kuhifadhiwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Lindi (Sokoine) mjini Lindi, ukisubiri ndugu na jamaa wautambue na kuchukua kwa ajili ya mazishi.

Mande alitoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi mwao kwa kuwa kama kijana huyo ni kibaka, angelisaidia Jeshi la Polisi kuwataja wenzake wanaoshirikiana nao katika vitendo hivyo.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Alexander Makalla, pia alithibitisha kupokewa mwili wa kijana huyo hospitalini huko, ukipelekwa na askari wa Jeshi la Polisi.

Dk. Makalla aliwaomba ndugu kufika hospitalini huko kuchukua mwili wa kijana huyo kwa ajili ya maziko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live