Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linamshikilia Ramadhan Nombo (18) mkazi wa Mtaa wa Sokoine Kata ya Kizota jijini Dodoma kwa tuhuma za kumuua, Livinus Pengo (23) akidaiwa kumchoma kwa kisu mkononi, kifuani na shingoni wakati akiamulia ugomvi.
Akizungumza leo Jumamosi Januari 7, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amesema tukio hilo lilitokea Januari 2 mwaka huu katika Mtaa wa Sokoine, Kata ya Kizota jijini Dodoma. Amesema mara baada ya tukio hilo wamemkamata mtuhumiwa huyo.
"Tunamshikilia mtuhumiwa na tunaendelea na upelelezi kujua shida ilikuwa nini," amesema Kamanda Otieno.
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa shuhuda, Mwadawa Egina amedai Januari 2 mwaka huu saa 1 usiku alisikia kelele nje ya nyumba yake.
Amedai alipotoka aliwakuta vijana watatu wakigombana huku Nombo akiwa na kisu. Egina amedai kuwa Livinus Pengo (marehemu) alikuwa akiwasihi wasigombane kwani wao ni marafiki, lakini ghafla Nombo alichomoa kisu na kumchoma shingoni na kifuani.
"Alipiga magoti chini akasema mbona unanichoma kisu huku akiniangalia mimi, wakati akisema hayo Nombo ndio akamchoma shingoni na kukivuta kisu hali iliyofanya damu kuruka juu," amedai shuhuda huyo.
Amedai kuwa marehemu alikuwa akiishi nyumba ya jirani na alikuwa akidai kuwa mwenyeji wa Jiji la Dar es Salaam.
"Marehemu alikuwa mtu mzuri, amechomwa visu hapa nje nyumbani kwangu na mimi nimeliona tukio mwanzo hadi mwisho, vijana wanashida kubwa sana.
"Nilimchukua nikampeleka hospitali, lakini damu zilikuwa zimetoka kwa wingi hasa kisu cha shingoni kilichoma kwenye mishipa ndio maana damu iliruka juu," amedai Mwadawa.
Mwili wakaa siku tano mochwari
Katika hatua nyingine mwili huo umekaa kwa siku tano mochwari tangu Januari 2 mwaka huu kutokana na ndugu kutojitokeza.
Mmoja wa rafiki wa marehemu, Abdul Changala amesema sababu ya mwili huo kukaa ni kutokana na ndugu kutojitokeza.
Amesema marehemu alikuwa fundi magari na akidai ni mwenyeji wa Dar es Salaam na wamejaribu kuwatafuta ndugu zake bila mafanikio.