Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Atangaza Wilaya ya Nyasa lango la kiuchumi

76c323a0e78bf0e81781f2aca24155f4 Atangaza Wilaya ya Nyasa lango la kiuchumi

Sun, 10 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Isabela Chilumba, ameitangaza wilaya hiyo kuwa lango kuu la kiuchumi baada ya serikali kuanzisha safari za meli za abiria na mizigo zinazofanya safari kati ya Mkoa wa Mbeya na Mbambabay wilayani humo kupitia Ziwa Nyasa.

Alisema mbali na usafiri wa meli, pia kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Mbambambay kunatajwa kuchochea maendeleo na kuharakisha kukua kwa uchumi wa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa jumla.

Chilumba alisema hayo juzi alipozungumza na wakazi wa Nyasa waliofika katika Bandari ya Mbambaby baada ya meli ya Mbeya 11 kuwasili katika bandari hiyo.

Meli hiyo ni kati ya meli tatu zilizotengenezwa na Serikali kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri katika Ziwa Nyasa.

Aliwahimiza wafanyabiashara wakubwa na wadogo wilayani humo, kuchangamkia fursa ya kuanza kwa safari za meli na zile zinazopatikana katika wilaya kwa kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa hoteli na viwanda ili kujiongezea kipato.

“Nawaomba sana ndugu zangu wa Mkoa wa Ruvuma na Watanzania wote kuchangamkia fursa ya kuimarika kwa usafiri katika wilaya yetu na hivyo, kuanzisha miradi mbalimbali itakayochochea kukua kwa uchumi wa familia na nchi kwa jumla,” alisema.

Akaongeza: “Serikali imeshatimiza wajibu wake kuanzisha safari za meli katika Ziwa Nyasa kilichobaki sasa ni kwetu sisi wananchi kuhakikisha tunachapa kazi na kutumia fursa zilizopo kujiongezea kipato.”

Aidha, alipongeza ujio wa meli hizo wilayani humo akisema utasaidia kukua kwa uchumi hasa ikizingatiwa kuwa Nyasa ni kitovu cha uchumi na biashara katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania baada ya kutajwa kuwa ni sehemu ya ukanda maarufu wa Ushoroba wa Mtwara, hivyo ni vyema wakazi wa Mkoa wa Ruvuma wasikubali kubaki nyuma kutumia meli hizo.

Alisema, kwa kawaida usafiri wa meli ni wa gharama nafuu ukilinganisha na usafiri mwingine.

Aliwahimiza wananchi kutumia zaidi meli kusafirisha bidhaa zao mbalimbali badala ya kubweteka na kuwaacha wageni wakinufaika na fursa hizo.

Mmoja wa maofisa wa meli ya MV Mbeya 11, Alex Masimba, alisema meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 150 na tani zaidi ya 200 za mizigo ambapo.

Kwa mujibu wa Masimba, kwa wiki watakuwa wanafanya safari moja kutoka Mbeya kwenda Mbambabay wilayani Nyasa.

Alisema, serikali imetengeneza meli tatu ambazo zimeanza kutoa huduma za usafiri katika Ziwa Nyasa ili kuboresha na kurahisisha maisha ya wananchi kwa gharama kidogo ya Sh 15,000; 35,000 na 45,000 kwa safari moja kutoka Mbambabay kwenda Mbeya.

Mkazi wa Mbambabay, Hairumu Malugu aalimshukuru Rais John Magufuli kwa kutengeneza meli zilizomaliza kero ya usafiri kwa wananchi wa wilaya hiyo na wakazi wa mkoa jirani wa Mbeya wanaotegemea ziwa kwa usafiri.

“Tulikuwa tunapata tabu sana tunapotaka kusafiri na kusafirisha mizigo kwa njia ya meli na barabara, lakini kuwepo kwa safari za meli za uhakika na kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami sasa kutabadilisha maisha ya watu wa Nyasa na Mkoa wa Ruvuma kwa jumla,” alisema Malugu.

Chanzo: habarileo.co.tz