Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Atakayehama kwa hiari Ngorongoro kulipwa Tsh mil. 10

Ngorongoro 71056561 Atakayehama kwa hiari Ngorongoro kulipwa mil. 10

Mon, 8 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wafugaji wa jamii ya Kimasai waliokubali kuhama Hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari kwenda Msomelo, Tanga, wanatarajiwa kulipwa fidia ya Sh. Milioni 10 kwa mali watakazoziacha kutokana na mchakato huo.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Mobhare Matinyi, alisema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumzia masuala mbalimbali.

Alisema serikali inajenga josho na eneo la malisho, bwawa la kunyweshea mifugo, mnada wa kisasa na vituo vya kupokelea maziwa.

Pia alisema kila atakayehama kupewa nyumba ya vyumba vitatu itakayokuwa katika eneo la hekari mbili na hekari tano za shamba na kwa wenye makaburi kufidiwa.

Akizungumzia kuzorota kwa huduma za kijamii Ngorongoro, Matinyi alisema, “Hakuna sababu ya kuongeza huduma wakati watu wanahama. Jambo la wazi unahamisha watoto wa shule unataka kuongeza shule haiwezekani.

“Tatizo kuna baadhi ya watu na asasi ambazo zinasambaza maneno ya uongo huduma zitaendelea kupanuliwa Msomelo ambako watu wanahamia na sio kule watu wanakohama,” alisema.

Kuhusu madai ya baadhi ya hospitali kudaiwa kuwatoza fedha wajawazito alisema: “Ni kweli kuna shida tumekuwa tukizisikia, Wizara ya Afya ina kitengo maalumu kinachofuatilia kila kifo cha mjamzito, pona yao ni pale wananchi watakapomfichia siri.

“Wananchi wasiogope kutoa taarifa, tunapojenga hizi zahanati na vituo vya afya tunataka kuona wanapatiwa huduma kwa kuzingatia weledi.”

Hata hivyo alisema katika kipindi cha miaka miwili serikali imeongeza vituo vingi vya afya kutoka vituo 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 9,366 mwaka 2023, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 9.6, jambo ambalo ni mafanikio makubwa.

Alisema ongezeko hilo, linajumuisha hospitali 436, vituo vya afya 1,126 na zahanati 7,804, sawa na ongezeko la vituo 817 ndani ya miaka miwili.

“Vituo vya afya vya kufanya upasuaji vilikuwa 340 hadi sasa vimefikia 523, sawa na ongezeko la asilimia 25, pia kuna ongezeko la vitanda vya kutolea huduma hali iliyoongeza ufanisi katika huduma ya mama na mtoto.

“Tungependa akina mama wanapokwenda kujifungua wasikabiliwe na tukio la kupoteza watoto lengo letu ni kufikia adhma ya vifo sifuri vitokanavyo na uzazi” alisisitiza.

Alisema vipaumbele vya sekta ya afya ni kuendelea kuimarisha huduma za afya katika mikoa na halmashauri zote nchini.

“Kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, kuongeza watumishi wa afya katika hospitali zote, ninawataka wananchi kutoa taarifa wanapoona hawatendewi haki katika vituo vya afya,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live