Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ataka vikundi kuanzisha viwanda kupata mikopo mikubwa

52e75d0493af901a8c00021b63343fc2 Ataka vikundi kuanzisha viwanda kupata mikopo mikubwa

Thu, 8 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji Kondoa, Msoleni Dakawa amevishauri vikundi vilivyonufaika na mikopo itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kujiunga na kuanzisha kampuni na viwanda vidogo ili kupata mikopo mikubwa na kujiimarisha kiuchumi.

Dakawa alisema hayo juzi wakati wa kikao cha kuvipongeza vikundi vilivyowahi kunufaika na mikopo na kukuza mitaji yao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano katika ofisi za Halmashauri hiyo.

" Mmehitimu nawapongeza sana, mkawe mfano na walezi wa vikundi vilivyoanza kupewa mikopo ili fedha walizopata wasije kupeleka kwenye sherehe ikiwa lengo lake ni kuwekeza ili wakue kiuchumi na kuendeleza familia na inawezekana kwa sababu fedha hizo wanarudisha bila riba,"alisema Mkurugenzi Dakawa

Aidha alisema kwa kuwa vikundi hivyo vimekua kimtaji na mapato yameongezeka hivyo ni wakati wao kulipia leseni ya biashara ambayo wanaweza kuitumia kupata mikopo benki, itakayowawezesha kukuza mitaji yao na si kitambulisho cha ujasiriamali kama awali ambacho kitabaki kwa ajili ya wajasiriamali wadogo.

"Fedha mlizokuwa nazo baada ya kumaliza mkopo zitumieni kwenye uwekezaji ikibidi fungueni kampuni au viwanda vidogo ambapo mtaajiri watu wengine nasi kama Halmashauri tutawaongezea mtaji hata milioni 20 kuliko fedha mlizokuwa mnazipata awali kama kikundi,"alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mohamed Kiberenge na Makamu Mwenyekiti, Besela Maunga wamewapongeza wanufaika hao kwa kufikia hatua hiyo na kuwashauri kuwatumia wataalamu wa Halmashauri katika miradi wanayotarajia kuwekeza.

Mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo, Hawa Chora ameishukuru Halmashauri kwa kuwawezesha fedha na mafunzo mbalimbali kutoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yamewasaidia kusimamia vizuri miradi yao na kukua kiuchumi.

"Sisi kikundi chetu awali tulianza na ufugaji wa nyuki, tukaingia kwenye kilimo cha alizeti ambapo kwa sasa tumejiingiza pia katika kazi ya kutengeneza majiko na maisha yetu kwa kiwango kikubwa yamebadilika nawashauri wataopata na waliopata mikopo hivi karibuni walipe marejesho kwa wakati ili wengine nao wanufaike,"amesisitiza Hawa

Awali akisoma taarifa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Irene Mosha alisema jumla ya vikundi 25 vimefanikiwa kurejesha mikopo yao vizuri na kukuza mitaji yao ambapo wanatarajia kuongeza mitaji zaidi kwa kukopa benki.

Halmashauri ya Mji kondoa imefanya kikao cha pamoja na wanufaika hao ikiwa ni pamoja na viongozi wa vikundi vilivyopata mkopo katika robo ya pili kwa mwaka 2020/2021 pamoja na wawakilishi wa Benki za CRDB, NMB na TPB waliotoa elimu ya manufaa na kuonesha fursa ya mikopo ya benki.

Chanzo: www.habarileo.co.tz