Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu azikwa na mamia, aacha watoto 18 wajukuu 12

60168 MOLLEL+PIC

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mererani. Katibu mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Raymond Mwangwala ameungana na wakuu wa wilaya za Arumeru na Hai mkoani Kilimanjaro katika mazishi ya mmiliki wa mgodi wa Tanzanite, Thomas Mollel maarufu Askofu.

Mazishi hayo yaliyofanyika kata ya Mbuguni mji mdogo wa Mererani wilayani Simanjiro, yalihudhuriwa na mamia ya wakazi wa eneo hilo.

Mollel alifariki dunia Mei 20 jijini Dodoma alipokwenda kumsindikiza kuapishwa mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki, Dk John Pallangyo.

Akiongoza ibada ya mazishi, mkuu wa Jimbo la Kusini Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), mchungaji Zakayo Palangyo alisema ndugu wanapaswa kuonyesha upendo kwa kushikamana wakati huu wa msiba.

Awali, mtoto wa marehemu, Onesmo Mollel akisoma wasifu wa baba yake, alisema alizaliwa mwaka 1951 na kupata watoto 20 kati yao, wawili walifariki dunia hivyo ameacha 18 na wajukuu 12.

Onesmo alisema baba yao alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa sukari na shindikizo la damu.

Pia Soma

Salamu za rambirambi

Wakitoa salamu za rambirambi, mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro alisema Mollel alikuwa mpenda maendeleo na alishawahi kumiliki timu ya mpira ya Pallson.

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Dk Pallangyo alisema kifo hicho kimemgusa sana kwa sababu hakuwa rafiki bali ndugu na hadi anafariki alikuwa amemsindikiza kuapishwa.

Naye katibu wa CCM wilaya ya Meru, Shaaban Mdoe alisema chama hicho kimempoteza mjumbe shupavu wa kamati ya siasa wilaya ya Meru na mjumbe wa halmashauri kuu wilaya.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mbuguni, Willy Melanyi alisema wakazi wa eneo hilo wamepata pigo kubwa kwani Mollel alikuwa mtu mwenye mapenzi mema na wananchi wa eneo hilo.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya; mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Loota Sanare; katibu wa CCM mkoa wa Arusha, Mussa Matoroka; na aliyekuwa mbunge Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.

Chanzo: mwananchi.co.tz