Mwanza. Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Flavian Kasala amekitaka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine kutumia miaka 20 ya kuanzishwa kwake kama kioo cha kujitathimini kule walikotoka na wanakoelekea.
Amesema kujitathimini huko kujikite katika masuala yote ya kiutendaji ikiwemo suala la kutoa elimu na la kiroho kama lilivyo lengo la chuo hicho.
Akihubiri katika misa takatifu leo Jumanne Julai 2, 2019 ibada iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwemo Rais mustaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, Askofu Kasala amesema mtu yeyote asiyefanya tathimini hawezi kujua mwelekeo wa maisha yake na wakati mwingine anajikuta anafanya mambo yasiyompasa kufanya.
"Katika maisha ya kawaida ni lazima ufanye tathimini ili uweze kufanya vitu vya heshima kwa kuwasamehe waliowakosea, kupongezana na kukosoana," amesema Askofu Kasala
Katika hatua nyingine, amekitaka chuo hicho kuangalia kisije kukumbwa na mambo ya kidunia na kujikuta wakijikita katika kutoa elimu pekee na kusahau masuala ya kiroho.
"Tutumie miaka 20 kufanya tathimini na kutafakari utendaji wetu na kumshukuru Mungu kwa watu wote waliochangia kuhakikisha chuo kimefika hapo kilipo," alisema Kasala
Pia Soma
- Takukuru yabaini kasoro miradi ya maendeleo Ilala
- Mwili wa mzamiaji wa ndege kutoka Kenya waanguka ikitua London
- UDSM waongeza muda wa juisi ya miwa kutumika
Amesema chuo hicho kimekuwa kituo cha muungano wa makabila na mataifa mbalimbali na kimefanikiwa kuhitimisha zaidi ya watu 30, 000 ambao wengi wamerudi chuoni hapo kutoa shukrani.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea katika sherehe hiyo