Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari polisi auawa vurugu mgodini

Anusurika Mgodi Pic Askari polisi auawa vurugu mgodini

Sat, 24 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vurugu zinazodaiwa kutokea katika mgodi wa dhahabu unaomilikiwa na kampuni ya Shanta, Ikungi mkoani Singida, baada ya kuvamiwa na zaidi ya wananchi 50, zimesababisha kifo cha askari polisi, Konstebo James Msesi.

Askari huyo anadaiwa kufariki dunia baada ya kupigwa risasi na mwenzake wakati akiwatawanya wananchi hao waliokuwa na silaha za jadi, waliovamia kibanda chao mgodini hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo huku akisema kundi la wananchi hao lilivamia kibanda cha askari hao juzi usiku wakiwa na silaha za jadi, ikiwamo mikuki.

“Mcheki RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) mchana atakuwa na taarifa kamili za tukio maana alikesha wilayani kwangu kwa ajili ya kushughulikia tukio hilo,” alisema Apson, akibainisha kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Meneja Mkuu wa mgodi huo, George  Kondela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea juzi saa 5:00 usiku mgodini hapo katika kijiji cha Sambaru, Kata ya Mang'onyi na kusisitiza kuwa maelezo zaidi yatatolewa na Jeshi la Polisi mkoani Singida.

“Hili ni tukio la kihalifu na tukio lolote la kihalifu lazima liripotiwe kwenye vyombo vya ulinzi na usalama. Ninakushauri ufike katika ofisi ya RPC au kwa OCD Ikungi (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) limesharipotiwa huko kwao na wao ndio wanaopaswa kutolea maelezo ya tukio hilo,” alisema.

Kamishna wa Madini Mkoa wa Singida, Sabai Nyansiri, alipoulizwa alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema amezipata kutoka kwa Meneja Mkuu wa Mgodi wa Shanta.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa, alipofuatwa na gazeti hili eneo la makazi ya nyumba za askari polisi, Mtaa wa Utemini, Manispaa ya Singida, ambapo shughuli za kuuaga mwili wa marehemu zilifanyika, alisema hayuko tayari kutoa taarifa zaidi kutokana na maelekezo kutoka ngazi za juu.

Hata hivyo, taarifa ambazo gazeti hili imezipata kutoka eneo la tukio, zilisema kundi la wananchi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 50 wakiwa na silaha mbalimbali za jadi, walivamia kibanda kimojawapo kilichoko eneo la  mgodi, ambacho kinatumiwa na askari polisi na walinzi wa mgodi.

Wananchi hao, kwa mujibu wa traarifa hizo, walianza kushambulia kwa mawe askari wawili waliokuwapo kibandani hapo na ndipo askari mwenzake aliyekuwa na silaha aina ya SMG alitoka na kukimbia mbali na kumwacha mwenzake  eneo hilo.

Askari huyo mwenye silaha (jina tunalo) baada ya kuona wananchi waliovamia wanaendelea kushambulia kwenye kibanda hicho, alipiga risasi hewani kuelekea kwenye kibanda kwa nia ya kuwatawanya lakini bahati mbaya baadhi ya risasi zilimpata askari mwenzake, hivyo kupoteza maisha.

Askari huyo aliyefariki dunia ni wa Kikosi cha Kutukiza Ghasia (FFU) cha mjini Singida na ana wiki chache tangu amehamishwa kutoka wilaya ya Mkalama kupelekwa Singida mjini.

Waziri wa Madini, Antony Mavunde, alipofanya ziara katika mgodi huo Oktoba, mwaka jana, aliwataka wamiliki wa migodi nchini kujenga uhusiano mzuri na jamii inayowazunguka na kuwasaidia kuwainua kiuchumi kwa kununua bidhaa wanazozizalisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live