Mkaguzi wa Polisi aliyekuwa akifanyakazi wilayani Arumeru, Stewart Kaino (47), amefariki dunia baada ya kuruka ukuta wa gesti na kuchomwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Taarifa za awali kutoka kwa shuhuda wa tukio hilo aliyeomba jina lake lihifadhiwe, zimedai kuwa Kaino aliingia katika nyumba hiyo majira ya saa sita usiku akiwa na mwanamke mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana.
Alisema aliandikisha katika kitabu cha wageni na kupewa chumba na kisha kuingia na mwanamke huyo, akiwa ameshika begi dogo la mgongoni na redio ya mawasiliano aliyokuwa nayo mkononi.
Alisema majira ya saa tisa usiku alitoka ndani ya chumba hicho na kumuacha mwanamke huyo akiwa amelala.
Alidai kuwa alikwenda nyuma ya nyumba hiyo na kuruka geti akiwa na lengo la kumtoroka mwanamke huyo ndipo alipoanguka na kuchomwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Taarifa zinadai baada ya mlinzi kusikia kishindo alienda katika geti hilo na kumkuta akiwa ameanguka chini akivuja damu nyingi kwenye paji la uso na kutoa taarifa polisi na majira ya alfajiri walifika na kukuta ameshapoteza maisha.
Alidai askari polisi walipekua begi la marehemu na kukuta chupa ya bia, chips, redio ya mawasiliano, simu mbili ikiwamo ya mwanamke huyo na vitu vingine.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai Jeshi la Polisi lilipokea taarifa Januari 8, mwaka huu majira saa 8:30 usiku.
Alisema taarifa hiyo ilieleza kuna mtu alifariki nje ya nyumba ya kulala wageni iliyopo Kata ya Levolosi jijini humo.
"Baada ya kupata taarifa hizi askari wangu walienda eneo la tukio na kukuta mwili ambao waliutambua kuwa ni Mkaguzi wa Polisi, Stewart Kaino (47) anayefanya kazi wilayani Arumeru," alisema.
Aidha, alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kubaini mazingira ya kifo hicho. Mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda kwao Bukoba kwa ajili ya maziko.