Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari JWTZ amepiga, amjeruhi dereva wa basi

Polisi Ytree Ajali Askari JWTZ amepiga, amjeruhi dereva wa basi

Fri, 26 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dereva wa basi la Saratoga linalofanya safari kati ya Dar es Salaam na Kigoma, Yassin Shabani, amejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Pwani, Tumbi, baada ya kupigwa na askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Tukio hilo linaelezwa kutokea juzi majira ya saa 1:30 asubuhi katika eneo la Kibaha Kwa Mathias baada ya Shabani (45) aliyekuwa akiendesha basi la Saratoga lenye namba za usajili T 555 DCZ kushambuliwa na kupigwa na askari huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi (ACP) Pius Lutumo, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo. Alisema mtuhumiwa ambaye ni askari wa JWTZ, Koplo Emmanuel Peleka, alimshambulia dereva huyo na kumsababishia kushindwa kuendelea na safari.

Kamanda Lutumo alisema kutokana na tukio hilo, Shabani alilazimika kwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Tumbi.

Lutumo alisema chanzo cha tukio hilo ni Koplo Peleka ambaye ni dereva wa gari la jeshi, kujaribu kulipita basi la Saratoga na kuwekewa pingamizi, jambo ambalo lingesababisha ajali, hivyo kusababisha taharuki iliyosababisha ugomvi baina yao.

Kamanda Lutumo alibainisha kuwa tayari hatua za kisheria zimechukuliwa kwa kumhoji mtuhumiwa na kupata maelezo ya mwathirika.

Kutokana na tukio hilo, Lutumo alitoa wito kwa madereva kutii sheria za usalama barabarani ili kuepusha taharuki na ajali zinazoweza kusababisha madhara na kusisitiza kuwa mbele ya sheria, wote wako sawa na hakuna aliye juu ya sheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live