Kijana anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 27 ambaye jina na eneo analotoka haijafahamika amevamia na kuharibu kwa kuvunjavunja mali kadhaa ikiwemo Altare ya Kanisa Kuu Jimbo Katoliki Geita.
Akizungumza na Waandishi wa habari mjini Geita leo Jumapili Februari 26, 2023, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Flavian Kasala amesema mtu huyo alioyejipenyeza ndani ya eneo la Kanisa kwa kuvunja kioo cha lango kuu pia amevunjavunja eneo la kuhifadhia sakramenti.
Askofu Kasala amesema kijana huyo ambaye tayari anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano ameharibu kiti cha Kiaskofu chumba cha ambacho Maskofu na Mpadre wanafanyia maandalizi kabla ya ibada.
“Mtu huyo ambaye hadi sasa hatujafahamu sababu za uvamizi wake pia aliharibu kwa kuvunja vitu na vifaa mbalimbali ikiwemo misalaba, sanamu za kiimani na vyombo vya kuhifadhia maji ya Baraka ambayo pia aliyamwaga,” alisema Askofu Kasala
Akizungumzia tukio hilo lililotokea Saa 8:00 usiku wa kuamkia leo Jumapili Februari 26, 2023, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay amesema kijana huyo anashikiliwa kwa mahojiano zaidi.
"Hadi sasa, Polisi tunawashikilia watu wawili kwa mahojiano akiwemo mlinzi aliyekuwa zamu usiku wa tukio. Taarifa zaidi nitazitoa kesho," amesema Kaimu Kamanda Mlay
Kwa mujibu wa Askofu Kasala, kabla kuharibu mali na samani za Kanisa, kijana huyo aling’oa kamera za ulinzi na usalama na kuharibu kifaa cha kuhifadhi kumbukumbu za matukio.
“Uvamizi na uharibifu uliofanyika siyo tu umesababisha madhara ya kiimani, bali pia hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya Sh20 milioni," amesema Askofu Kasala
Amesema hadi sasa, bado haijafahamika namna gani kijana huyo alifanikiwa kuvamia eneo la Kanisa lenye ulinzi kwa Saa 24.
Muumini wa Kanisa Katoliki mjini Geita, Salome Boniphace amefaninisha uvamizi na uharibifu uliofanyika na kufuru kwa sababu maeneo yaliyoguswa yanahesabika kuwa ni Takatifu kiimani.
"Hii ni kufuru kwa imani; na kibaya zaidi ni kitendo hiki kimefanyika usiku wa kuamkia Ibada ya Jumapili ya kwanza tangu tuanze mfungo wa Kwaresma,” amesema Salome akiviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua za kisheria.