Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 90 Singida wanasoma darasani wakiwa na njaa

Ffd2ddb260a388028a0697f15387192f.jpeg Asilimia 90 Singida wanasoma darasani wakiwa na njaa

Sun, 24 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Zaidiya asilimia 90 ya shule za msingi za serikali ndani ya Manispaa ya Singida hazitoi chakula cha mchana kwa wanafunzi wake, hali inayoathiri usikivu, umakini, uelewa na ufaulu hasa kwa watoto chini ya miaka nane ambao bado wanahitaji lishe bora kwa ajili ya ukuaji wa ubongo wao ili waweze kufanya vyema darasani.

Katika taarifa yake, Ofisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Singida, Eugene Shayo anasema kati ya shule 50 za serikali, ni nne tu ndizo zinatoa chakula kwa wanafunzi lakini shule za binafsi zote 16 zinatoa huduma hiyo.

“Sababu ya shule nyingi za serikali kutowapatia chakula wanafunzi ni wazazi kukataa kuchangia wakati hizo nne zinatoa chakula ni kutokana na kuwa na wanafunzi wenye mahitaji maalumu, hivyo serikali hubeba mzigo huo,” alisema Shayo na kuongeza kuwa shule binafsi ni lazima zitoe chakula kwa kuwa wazazi wanalipa ada.

Alikiri kuwa kiwango cha ufaulu darasani kwa wanafunzi wanaopata chakula cha mchana ni kizuri zaidi ikilinganishwa na wale wasiopata chakula.

Mmoja wa walimu wanaofundisha chekechea ambaye hakupenda jina lake litajwe alisema hali ni mbaya zaidi kwa wanafunzi wadogo walio chini ya miaka nane ambao licha ya kuwahi kutoka shuleni, mara nyingi ikifika saa nne tu asubuhi huwa wanaanza kusinzia kwa njaa na uchovu hivyo kukosa usikivu.

“Kwa hivi vitoto vya chekechea vilivyopo shule za serikali hali ndio mbaya zaidi kwani ikifika mchana utavihurumia, vyote utakuta vinasinzia na kupiga miayo kwa njaa na uchovu,” alisema na kuongeza kuwa kuna haja ya serikali kuchukua hatua katika suala hilo ili watoto wote wapate lishe shuleni.

Mmoja wa wazazi, mkazi wa Ipembe Singida mjini, Hatibu Ismail alisema kuwa tatizo sio wao kugoma kuchangia bali viongozi na watendaji kushindwa kutimiza vyema wajibu wao wa kuhamasisha juu ya umuhimu wa suala hilo kwa maendeleo ya mwanafunzi shuleni.

Mtaalamu wa lishe Mkoa wa Singida, Teda Sinde alisema kuwa ulaji duni au ulaji usiozingatia makundi matano ya chakula huathiri ukuaji wa ubongo hivyo kusababisha mtu kutokufundishika kirahisi na kuwa mzito kwenye kufikiria na kutoa uamuzi, pia husababisha upungufu wa damu mwilini.

Alisema kuwa lishe duni huathiri mfumo wa kinga ya mwili katika kupambana na magonjwa, mtoto kupata utapiamlo na magonjwa mengine hadi kusababisha vifo.

Takwimu za utafiti wa kitaifa za mwaka 2018 juu ya hali ya lishe mkoani Singida zinaonesha kuwa asilimia 29.8 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana udumavu, asilimia tano ukondefu na asilimia 15 wana uzito mdogo.

Aidha, utafiti huo unabainisha kuwa asilimia 27.9 tu ya watoto hao ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na asilimia tatu ya watoto walio chini ya miaka miwili ndio angalau hupata mlo unaokubalika katika tafsiri ya lishe bora.

Chanzo: www.habarileo.co.tz