Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 80 ya wanaomaliza kidato cha nne hufeli somo la hesabu

14528 Hesabu+pic TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako amewataka wataalamu wa hisabati kuja na mbinu zitakazomaliza tatizo la wanafunzi wengi kufeli somo hilo.

Amesema inasikitisha kuona ufaulu wa hisabati katika kipindi cha miaka kumi iliyopita hauvuki asilimia 20.

Akizungumza leo Agosti 29  na wataalamu wa hisabati kutoka nchi mbalimbali duniani katika kongamano  linalofanyika Chuo Kikuu cha Aga  Khan, jijini Dar es Salaam, Profesa Ndalichako amesema ni aibu kuona asilimua 80 ya wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne kila mwaka wanafeli hesabu.

"Serikali hatuwezi kuendelea luangalia asilimia 80 ya wanafunzi wakifeli hesabu kila mwaka, nataka wataalamu muangalie tatizo lililopo kwenye ufundishaji, kwanini wanafunzi wafeli hivi?" amesema.

Amesema mtandao wa kufeli hisabati unatokana na idadi ndogo ya walimu wanaozalishwa kufundisha somo hilo kwa sababu wanafunzi wengi wanalikimbia.

"Nataka tuuvunje huu mtandao, kama wanafunzi watakimbia hesabu wale wachache wanaobaki wakisomea ualimu hawawezi kukidhi mahitaji, mwisho bado tutaendelea kuwa na uhaba wa walimu kila mwaka," ameeleza Profesa Ndalichako.

Amesema Serikali imedhamiria kuboresha elimu na walimu wa hesabu wanawajibj wa kuwekeza katika kuwasaidia watoto wajue kukokotoa somo hilo.

Mkuu wa Chuo cha Aga Khan Profesa Joe Lugalla amesema tatizo kubwa la hisabati sio wanafunzi ni ufundishaji.

"Ndio maana tupo hapa, tunataka kujadili mbinu na mikakati yetu katika kuona kila mtoto anaweza hesabu," amesema.

Amesema katika mkutano huo watapeana mbinu na uzoefu kutoka nchi mbalimbali namna wanavyoweza kumaliza ugonjwa wa kukimbia na kuona somo hilo gumu.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Hisabati wa Aga Khan, Profesa Fredrick Mtenzi kwa sababu tatizo kubwa linaonekana kwenye ufundishaji, mbinu na mikakati inayoandaliwa ni kuona namna bora inayoweza kumfanya kila mwanafunzi kuona hesabu ni rahisi.

"Hata hii Tanzania ya viwanda inayosemwa kama wanafunzi hawajui hesabu sio rahisi kuifikia, tunataka kuona mtoto wa chekechea hadi chuo kikuu analifurahia somo hilo, sio gumu ni rahisi kabisa ila shida ipi kwenye ufundishaji," amesisitiza.

Amesema kinachohitajika ni mbinu mpya za ufundishaji unaoshirikisha wanafunzi wenyewe na kutumia mifano rahisi kutoka kwenye mazingira yanayowazunguka wanafunzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz