Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 50 ya miradi nchini ni ya wazawa

9689 Tic+pic TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kimesema asilimia 50 ya miradi yote iliyosajiliwa nchini ni ya watanzania, ikifuatiwa na asilimia 22 ya wageni na asilimia 23 ni ya ubia kati ya watanzania na wageni.

Meneja wa TIC kanda ya kaskazini, Daudi Riganda ameyasema hayo leo Agosti 2 wakati wa utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali waliofanyika kwenye maonesho ya nane nane jijini Arusha.

Riganda amesema kulingana na takwimu walizonazo miradi mingi ya kiuwekezaji nchini ni ile watanzania kwani wamechangamkia fursa ya uwekezaji na kusajili miradi yao kwenye sekta mbalimbali.

Amesema watanzania wamewekeza na kusajili miradi yao mbalimbali kwenye sekta za kilimo, mahoteli, viwanda vikubwa, vya kati na vidogo.

"Pia watanzania wengi wamechangamkia fursa ya uwekezaji wa ujenzi wa majengo ya biashara, mawasiliano kwa njia ya redio na televisheni, kompyuta, usafirishaji, uchukuzi na huduma mbalimbali," amesema.

Amesema lengo lao  ni kutoa elimu na kuwaamsha wafanyabiashara na wajasiriamali hao kuzitumia fursa mbalimbali za kiuwekezaji zilizopo kanda ya kaskazini yenye mikoa minne ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga.

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amewataka wananchi wa kanda ya kaskazini kutumia maonyesho hayo kwa ajili ya kuboresha uchumi wao kwa kujifunza namna wenzao wanavyofanikiwa kupitia sekta mbalimbali.

"Ukipita kwenye mabanda tofauti utapata elimu nzuri kama ni ufugaji au kilimo utaona kinavyofanyika kitaalamu na siyo kwa mazoea kama watu wanavyofikiri," amesema Mofuga.

Chanzo: mwananchi.co.tz