Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 13 wanajisaidia vichakani Geita

Vichakaniii Vyooo.jpeg Asilimia 13 wanajisaidia vichakani Geita

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Imeelezwa kuwa asilimia 13.4 ya wakazi mkaoni hapa hawana vyoo hali inayosababisha uwepo wa hatari ya magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu.

Mkoa huo wenye watu zaidi ya 2.97 milioni ni miongoni mwa mikoa ambayo baadhi ya watu wake hawana vyoo na takwimu zikionyesha asilimia 13.4 sawa na watu 398,999 wanajisaidia vichakani.

Aidha asilimia 18.5 sawa na watu 550,857 wanatumia choo kimoja kwa kaya tano au zaidi, huku asilimia 22 sawa na watu 655,073 ni kaya zenye vyoo ambavyo havijaboreshwa.

Kwa mujibu wa matokeo ya Utafiti wa Demografia na Afya na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022 yanaonyesha ni asilimia 46 pekee ya wakazi wa mkoa huo wenye vyoo vilivyoboreshwa.

Mganga Mkuu wa mkoa huo, Omari Sukari akizungumza na Mwananchi amesema hakuna tafiti zilizofanywa kujua sababu kwa nini baadhi ya watu hawana vyoo, lakini mila na tamaduni za jamii ya kanda hiyo zinaweza kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia watu kujisaidia vichakani.

Akizungumza hivi karibuni katika kikao cha tathmini cha huduma endelevu za upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira, Sukari amesema kama mkoa wameandaa mikakati ya kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora na kinatumika.

Mikakati

Ametaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii ili wajue vyoo bora ni vya aina gani, kazi itakayofanywa na maofisa afya, watendaji wa vijiji na kata.

Mkakati mwingine ni Halmashauri kutunga sheria ndogo za kulazimisha wananchi kuwa na vyoo bora.

“Tunawaeleza wananchi kwa nini kuna umuhimu wa kuwa na choo bora, lakini sio kuwa nacho tu kitumike pia maana kuna wengine watajenga na wataendelea kujisaidia vichakani.”

“Ili kupunguza magonjwa yatokanayo na uchafu wa mazingira kama homa ya matumbo, kuhara, kutapika, kipindupindu na mengine lazima watu watumie choo bora,” amesema Dk Sukari.

Amesema katika kukuza uelewa wa matumizi bora ya choo watashirikiana na walimu mashuleni ili wawafundishe wanafunzi, ambao nao watakwenda kutoa elimu hiyo kwa wazazi lengo likiwa ni kuboresha usafi wa mazingira.

Dk Sukari amesema mbali na kaya zisizo na vyoo lakini hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya uchimbaji madini na kwenye maeneo ya uvuvi, (mialo) ambayo yanakuwa na mikusanyiko ya watu wengi.

“Maeneo mengi ambayo hayana vyoo ni kwa wachimbaji wadogo na wavuvi kule mwaloni wao wanaona kwa sababu wanaingia na kutoka hawana sababu ya kuwa na vyoo, tayari tumeagiza maeneo yote yajengwe vyoo kwani wanajisaidia vichakani na kusababisha uchafuzi wa mazingira na maji," amesema Dk Sukari.

Amesema tayari familia ambazo hazina vyoo zimeanza kutozwa faini ya Sh50,000 na wale wanaokaidi watapandishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria ya afya ya jamii ya mwaka 2009.

Choo bora ni kipi?

Kwa mujibu wa Dk Sukari choo bora ni kile kilichoezekwa kwa bati, kujengwa ukuta imara unaweza kuwa wa tofali za saruji au udongo na chini kinapaswa kiwe na sakafu inayofaa kuosha kwa maji na kiwe na mfumo mzuri wa kutoa uchafu.

Kwa nini wananchi hawana vyoo?

Rehema Shija mkazi wa kijiji cha Ikurwa katika kata ya Ihanamilo Mjini Geita ambaye hana choo kwa zaidi ya miezi saba, amesema hulazimika kwenda kwa jirani na wakati mwingine kujisaidia shambani baada ya choo chake kutitia kutokana na mvua zilizonyesha.

Naye Juma Bakari, mkazi wa Mtaa wa Elimu kata ya Nyankumbu amesema licha ya choo kuwa ni cha muhimu kwenye jamii, lakini hali duni ya kimaisha imemfanya ashindwe nacho.

“Mimi nimechimba choo cha kawaida nimezungushia nyasi na kilitumika miezi mitatu tu kikajaa kutokana na udongo wa kichanga uliopo eneo hili na mvua zinazonyesha,” amesema Bakari

Aidha hali duni ya maisha ni miongoni mwa changamoto zinazowafanya washindwe kujenga vyoo imara kwani wengi hutegemea kilimo cha zao la pamba, ambacho sasa ni kama kimekufa.

“Kumwambia mwananchi akusanye laki saba ajenge choo bora ilihali hata pesa ya kula hana mlo mmoja anaipata kwa mawazo, sio rahisi," amesema Justin Mwanuka.

Diwani wa kata ya Ihanamilo, Joseph Lugaila amesema wananchi wake wanajitahidi kujenga vyoo lakini ni duni na mvua ikinyesha hutitia hivyo kushindwa kutumika.

Novemba 2023 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumzia matumizi ya vyoo bora nchini alisema yameongezeka kutoa asilimia 21 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 74.8 mwaka 2022, ikiwa ni hatua chanya ya kufikia lengo la 6.2 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya 2030.

Aliitaja mikoa inayoongoza kwa matumizi ya vyoo bora na asilimia zake kwenye mabano ni Dar es Salaam (98.5), Ruvuma (92.1), Njombe (87.6) huku mikoa inayoongoza kwa kutokuwa na vyoo ni Katavi (24.3), Simiyu (24.3) na Manyara (22.3).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live