Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asasi 26 zadai kunyimwa kibali kufuatilia uchaguzi Serikali za mitaa, Jafo ajibu

87247 Uchaguzipic Asasi 26 zadai kunyimwa kibali kufuatilia uchaguzi Serikali za mitaa, Jafo ajibu

Thu, 5 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Viongozi wa Mtandao wa Uangalizi wa Uchaguzi  Tanzania (Tacceo) wamedai kunyimwa vibali ya  kufuatilia mwenendo wa uchaguzi wa Serikali za mtaa licha ya kufuata taratibu na masharti.

Viongozi hao wa Tacceo inayojumuisha asasi za kiraia 26 za Tanzania bara na Zanzibar wametoa madai hayo leo Alhamisi Desemba 5, 2019 wakati wakitoa tathmini ya uchaguzi huo ambao CCM kiliibuka na ushindi wa zaidi ya asilimia 90.

Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo alipoulizwa kuhusu madai ya Tacceo amesema, “uchaguzi umeshamalizika kwa sasa  tunaendelea na ajenda  ya maendeleo. Wananchi wanatakiwa kwenda kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki vyema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.”

Jafo azijibu balozi za Marekani, Uingereza

Katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 24, 2019 vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, UPDP, ACT- Wazalendo na Chauma havikushiriki.

Mjumbe wa kamati ya uongozi wa Tacceo, Bubelwa Kaiza amesema walitimiza masharti kuangalia uchaguzi kama inavyoeleza Sheria ya Serikali ya Mitaa sura 287.

“Tacceo tuliomba vibali lakini tulinyimwa bila kupewa sababu za msingi. Uamuzi wa Serikali wa kutotupa kibali sio tu umeinyima Tacceo haki ya kuangalia bali umewanyima haki raia wa Tanzania kujua mwenendo wa uchaguzi kama ulikuwa huru na haki.”

"Tofauti na asasi nyingine  yoyote ya kiraia nchini,  Tacceo pekee ndio ilikuwa na mipango na maandalizi teknolojia, utaalamu na mtaji wa kijamii wa kuangalia  kwa ufanisi uchaguzi huu na kutoa ripoti huru inayoaminika kwa wadau," amesema  Kaiza.

Kaiza amesema kwa mazingira hayo ya kutokuwepo kwa uwazi unaoweza kuthibitishwa na waangalizi huru wa uchaguzi, wadau wa uchaguzi nchini wanashindwa kuthibitisha kwa uhakika iwapo uchaguzi wa Serikali za mitaa ulikuwa huru na haki.

"Kama tunavyojua kwenye uchaguzi ni kuchagua mtu mmoja baina ya washindani inakuwa vigumu kuthibitisha iwapo matokeo ya uchaguzi huu  yana akisi utashi wa mpiga kura,"amesema Kaiza.

Akitoa maoni ya Tacceo kuhusu uchaguzi huo, mwanachama wa mtandao huo Sophia Komba amesema kwa kuzingatia uchambuzi walioufanya wamebaini mchakato huo uligubikwa na kasoro za mifumo na kiutendaji zilizosababisha watu kunyimwa fursa ya kupiga kura.

" Ni dhahiri kuondolewa kwa wagombea kulisababisha wananchi kunyimwa fursa na haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa. Wagombea wengi bila kuwa na hadhi ya uongozi wa umma walipitishwa  kuongoza vitongoji, vijiji na mitaa bila kupingwa," amesema Komba.

Chanzo: mwananchi.co.tz