Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arusha wampongeza JPM kukemea ukabila

D2d048c6f581f3f8f5834b7ae6cbc25e Arusha wampongeza JPM kukemea ukabila

Sun, 25 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KAULI ya Rais John Magufuli aliyoitoa juzi ya kutaka wananchi wa Jimbo la Arusha Mjini kuacha kuchagua mgombea wa ubunge kwa kufuata ukabila imewagusa wengi ambao wamemuunga mkono wakitaka vitendo hivyo vikomeshwe mara moja.

Magufuli alitoa rai hiyo juzi wakati akiomba kura katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shekh Amri Abeid.

Mwanasiasa mkongwe jijini Arusha, Modest Meikoki alisema ukabila jijini humo ni kidonda ndugu kinachopaswa kupatiwa dawa na hilo linaweza kufanywa na Magufuli.

Meikoki ambaye aliwahi kuwa Diwani Kata ya Daraja Mbili, Naibu Meya Halmashauri ya Manispaa ya Arusha (sasa Jiji) na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) miaka ya 1980 hadi 2000, alisema ukabila uliwahi kukemewa na kupigwa vita na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema katika kipindi hicho cha Nyerere, baadhi ya viongozi wa chama waliokuwa wakiongoza ukabila walikatwa katika nafasi mbalimbali ndani ya chama.

Aliomba Magufuli atakapochaguliwa kuwa Rais, achukue hatua ndani ya chama kuanzia ngazi ya shina hadi wilaya katika jijini Arusha kukomesha hilo vinginevyo hali inaweza kuwa mbaya zaidi miaka ijayo.

“Mwalimu aliliona hilo na alionya na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na wale wanaoeneza ukabila kukatwa iwapo watawania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama na hilo linapaswa kuchukuliwa hatua za dhati sasa na mwenyekiti wa CCM Taifa kwani likienea linaweza kuwa sumu hapo baadaye,” alisema Meikoki.

Mkazi wa Arusha, James Rugangira alisema ukabila ni tatizo kubwa katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi mbalimbali za siasa mkoani Arusha na kwamba likikemewa, wanaweza kupata viongozi bora wa kuongoza jimbo hilo.

Alisema kwa kuwa Rais Magufuli ameliona, wananchi wa Arusha Mjini wanapaswa kubadilika na kukubali kuchagua mgombea wa kabila lolote ili mradi awe na uwezo,ushawishi na mpenda maendeleo.

Akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua ya kukabili ubaguzi huo, Semmy Kiondo alisema: “Ukitaka kuwa Mbunge jimbo la Arusha lazima uwe kabila (analitaja), ukitaka kuongoza chama lazima uwe kabila fulani bila ya hivyo hupati hapo ndipo penye shida hivyo hatua za haraka zinahitajika kukomesha hilo na Rais amepongezwa sana kwa kukemea hadharani.”

Chanzo: habarileo.co.tz