Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arusha wafaidi ushirikiano Tanzania, Marekani kiafya

A43cc51cb96cec9883f44fcfc625880b Arusha wafaidi ushirikiano Tanzania, Marekani kiafya

Fri, 4 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKOA wa Arusha ni miongoni mwa mikoa 12 nchini inayofaidika na ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Tanzania na Marekani katika masuala ya afya kwa akinamama na vijana.

Mkoa huo unanufaika na eneo hilo kupitia mradi wa USAID Tulonge Afya unaotekelezwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Shirika la FHI360 nchini.

Mradi wa USAID Tulonge Afya kupitia jukwaa la NAWEZA unatekeleza sherehe za akinamama wenye watoto chini ya miaka mitano kwa pamoja ili kujadiliana masuala yanayohusu afya ya mama na mtoto na kuwapa uzoefu wa jinsi ya kuwalea watoto ili wawe na afya njema.

Akizungumza katika katika sherehe hizo za akinamama, Mwakilishi wa Shirika lisilo la Kiserikali la EMAC, Dennis Kabuta, alisema juhudi kama hizo za Mradi wa USAID Tulonge Afya za kuwafikia akinamama zinaendana na juhudi za serikali za kupunguza vifo vya akinamama na watoto.

Aidha, aliwataka akinamama hao kufuata ushauri kuhusu matumizi ya huduma za afya ya uzazi sambamba na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya wanapoona dalili za homa kwa watoto.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk Donald Wright, alisema Marekani itaendeleza ushirikiano mzuri uliopo baina yake na Tanzania ili kuhakikisha huduma za afya zinazolenga miundombinu, rasilimali watu na mabadiliko ya tabia zinapewa vipaumbele.

Alisema Marekani inajivunia kazi nzuri zinazofanywa na wadau wake na kuutaja mradi wa USAID Tulonge Afya kama mfano wa kuigwa.

Balozi Wright alisema Marekani na Tanzania ni marafiki hivyo zitaendelea kushirikiana kuhakikisha vita dhidi ya malaria na virusi vya Ukimwi inafanikiwa kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARVs) kwa wanaoishi na VVU pamoja na kuwakinga wajawazito na watoto dhidi ya malaria.

Kwa mujibu wa Meneja Mradi wa USAID Tulonge Afya, Kanda ya Kati na Kaskazini, Japhet Daudi, sherehe hizo zinazofanyika kwa mfumo wa dhifa ya jikoni, huwakutanisha akinamama kujadili namna ya kutatua changamoto za malezi kwa watoto.

Alisema tangu mwaka 2019 hadi sasa mikutano 13 imefanyika katika Kanda ya Kati na Kaskazini na kuwafikia akinamama 682.

Mshiriki mmoja, Mariam Evance, alisema amefurahia zilivyoendeshwa hasa katika kuwakumbusha masuala mbalimbali ya kiafya kwa kuhakikisha afya za watoto wao zinaimarika.

Chanzo: habarileo.co.tz