Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Apewa figo na dada yake, akosa Sh50 milioni kuipandikiza

Figo Dada Yke Apewa figo na dada yake, akosa Sh50 milioni kuipandikiza

Tue, 4 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya dada yake kukubali kumchangia figo, maisha ya kijana Dickson Sambo aliyeishi miaka minane akisafishwa damu kutokana na tatizo la figo, bado yako kwenye hatihati.

Kijana huyo mkazi wa Mbokomu, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambaye figo zake zote mbili zilifeli miaka minane iliyopita, ameshindwa kupandikizwa ogani hiyo kutokana na kukosa Sh50 milioni za kugharimia upandikizaji.

Sambo amesema alifikia hatua ya kuuza mali zake zote ili apate fedha za kuchuja damu (dialysis) ambapo kila wiki husafisha damu mara tatu na gharama yake ni Sh200, 000 kwa siku.

Akizungumza na Mwananchi, kijana huyo amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan, kumsaidia aweze kupata Sh50 milioni kwa ajili ya upandikizaji wa figo, kutokana na hali mbaya ya uchumi aliyonayo baada ya kuuza mali zote kupigania afya yake.

"Mwaka 2017 nilipata tatizo la kufeli kwa figo zangu zote, nilishindwa kufanya kazi hivyo nikaanza kufanya dialysis (kusafisha damu) kwa kipindi chote hicho. Bahati nzuri ndugu wamejitolea kunisaidia figo, lakini tatizo nililonalo ni gharama (za upandikizaji), natakiwa niwe na Sh50 milioni kwa ajili ya upandikizaji," amesema.

Amesema imefikia mahali familia haina uwezo tena wa kumsaidia baada ya mali na fedha walizokuwa nazo kutumika kwenye matibabu ya kusafisha damu.

"Imekuwa ni ngumu kwetu kupata hizi fedha, maana tangu nipate hili tatizo nimekuwa nikienda kusafisha figo na kwa wiki inatakiwa niende mara tatu na kila nikienda ni Sh200, 000.

"Familia wamepambana na mimi kweli nashukuru Mungu katika kufanikisha haya matibabu, imeshahangaika, imeuza mali kwa ajili ya kunisaidia, hatuna kitu na tunakoelekea naona maisha yangu yanaweza kuwa hatarini," amesema Sambo.

Amewaomba Watanzania kumsaidia chochote ili apate fedha hizo ili kunusuru maisha yake.

"Naiomba Serikali yangu, Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu na Waziri wa Afya, kama viongozi wa Taifa mnisaidie kwenye hili niweze kupata hizi Sh50 milioni ili niweze kuondokana na tatizo hili.

"Hapa nilipo nina watoto wanne, mimi ndio baba nategemewa kila kitu kwenye familia yangu, nilivyokuwa navyo vyote nimeuza na sina msaada mwingine wowote wa kunisaidia, hata fedha za kwenda kusafisha figo nazo zimekuwa zikinipiga chenga, wakati mwingine nalazimika kwenda mara moja kwa wiki badala ya mara tatu.

"Nawaomba Watanzania wenzangu mnisaidie ili niweze kurudi katika afya yangu ya kawaida na niweze kuilea familia yangu kama mwanzo," amesema Sambo.

Jackline Sambo aliyejitolea kumsaidia figo kaka yake, amesema ameona amsaidie kwa kuwa ameteseka muda mrefu na kuwaomba Watanzania kumsaidia ndugu yake ili aweze kurejea katika afya yake ya kawaida.

"Ndugu yetu ameteseka tangu mwaka 2017 ambapo sisi kama familia tumepambana na tatizo lake kumuuguza kwa muda wote na kwa sasa sisi kama familia hali yetu imekuwa mbaya, hatuna chochote tena cha kusaidia kumuuguza."

"Kama mdogo wake, nipo tayari kumtolea figo kaka yangu ili aweze kuishi kama sisi tunavyoishi maana ameteseka sana. Ndugu zangu Watanzania kutokana na gharama hizi kuwa kubwa na kama familia tumeshindwa, tunaomba Watanzania wenzetu mtusaidie kwa chochote ili tuweze kugusa maisha ya ndugu yetu," amesema Jackline.

Chanzo: Mwanaspoti