Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aomba wahakiki wapewe ushirikiano kukamilisha utafiti

2f40548beeaf4eeadfbb1d3d8de6cdc4.png Aomba wahakiki wapewe ushirikiano kukamilisha utafiti

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAJUMBE wa serikali za vijiji wilayani Mbarali wanaoshiriki kwenye uhakiki wa kaya zinazonufaika na Mpango wa Kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(Tasaf) wametakiwa kutoa ushirikiano mzuri ili wawezeshaji wa mpango huo kutoa takwimu sahihi kwenye uhakiki wa awamu ya pili na ya mwisho.

Ofisa Ufuatiliaji wa Tasaf wilaya ya Mbarali, Lugembe Buyamba alitoa rai hiyo alipozungumzia hali ya uhakiki wa wanufaika wa Tasaf III baada ya kumalizika kwa kikao kazi kilicholenga kuweka mpango wa kuhakiki kaya nufaika zilizosalia kwenye uhakiki uliofanyika Julai, mwaka huu.

Buyamba alisema wajumbe watatu wa kila serikali ya kijiji ndiyo wanapaswa kuwasaidia wawezeshaji kupata taarifa zilizo sahihi kwa kuwa wao ni wenyeji zaidi.

Sambamba na hilo aliwasihi wawezeshaji kuwa makini kwenye maeneo wakitambua kuwa uhakiki unaofanyika awamu hii ni wa mwisho na hakutakuwa na uhakiki mwingine tena.

Aliwaonya wasije na taarifa zitakazosababisha wahusika kunyimwa haki za msingi.

“Lazima tujue kaya zipi zina watoto wanahudhuria kliniki, tujue kaya zipi zina watoto wanaokwenda shule. Na taarifa zitolewe na msimamizi wa familia na si kutuma mwakilishi au majirani. Na izingatiwe kuwa uhakiki huu ni wa kaya zinazoendelea kunufaika na kusiwe na mzozo wa kuingizwa kaya mpya.," alisisitiza.

Aliwasihi pia viongozi wa vijiji wakiwemo maofisa watendaji kutoa taarifa mapema kwa wananchi kwenye maeneo yao ili wanufaika waweze kujiandaa na kushiriki kikamilifu kwenye uhakiki.

Kwa upande wake, Mmoja wa wawezeshaji wa mpango huo, John Msechu alisema changamoto iliyojitokeza kwenye uhakiki wa awali ni pamoja na wanufaika kutumia mazoea na kutaka kuwakilishwa na majirani kutoa taarifa.

Alibainisha pia changamoto za wanufaika kutopata taarifa kwa wakati sambamba na jiografia ya maeneo isiyo rafiki kuwa ilichangia zoezi kufanyika kama lilivyopangwa na kusababisha baadhi ya kaya kutopatikana taarifa zake.

Chanzo: habarileo.co.tz